MTANGAZAJI WA IDHAA YA KISWAHILI DW MOHAMMED DAHMAN AFARIKI DUNIA


Mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW mjini Bonn Mohammed Dahman,amefariki dunia siku ya Ijumaa (02.08.2019) mjini Cologne, magharibi mwa Ujerumani.


Mohammed alikuwa mwandishi habari mahiri katika nyanja zote, lakini alipendelea sana taarifa ya habari za ulimwengu na makala ya mbiu ya mnyonge.

Asilimia kubwa ya wasikilizaji walizipenda sana makala zake kuhusu masuala ya haki za binadamu na sauti yake ya huruma. Aliwapa sauti wasiokuwa na saut, hakukata tamaa kuwatafuta watu muafaka wa kuwahoji na alikuwa makini sana katika kuhakikisha taarifa zake pamoja na makala haziegemei upande mmoja.

Kama mwandishi, Mohammed alikuwa mfano wa kuigwa kwa wengi wetu. Amekuwa akiugua kwa kipindi cha takriban miaka miwili na muda wote huu hakuweza kufanya kazi. Hata hivyo hatukukata tamaa kwamba angepata afueni na kurejea kazini kujumuika nasi kuendelea na majukumu yake.

Katika wakati huu mgumu wa majaribu, fikra na dua zetu tunazielekeza kwa mke wake, binti yake na familia yake visiwani Zanzibar na ughaibuni. Tunawapa pole na kutoa rambirambi zetu kwa majonzi makubwa, machozi yakitiririka machoni mwetu. Tunawaombea. Tulimpenda, lakini Mungu amempenda zaidi.

Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya DW, Andrea Schmidt, na wafanyakazi wote wa idhaa hii mjini Bonn tunawapa pole jamaa, marafiki na mashabiki kwa kuondokewa na mpendwa wetu. 

(Andrea Schmit; Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya DW)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527