BOMBA LA MAJI YA ZIWA VICTORIA LAUA TABORA



Kamanda Polisi Mkoa wa Tabora, Barnabas Mwakalukwa

Mtoto mmoja mwenye umri wa miaka 9 ambaye ni mwanafunzi wa Darasa la tatu katika Shule ya Msingi Kiyungi iliyopo Manispaa ya Tabora mkoani Tabora, amefariki dunia mara baada ya kuporomokewa/kukanyagwa na bomba kubwa la maji huku mwingine akijeruhiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Barnabas Mwakalukwa akizungumza leo Agosti 28 na EATV & EA Radio Digital, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amedai kuwa mabomba hayo ni ya mradi mpya wa usambazaji wa maji mkoani humo kutoka Ziwa Victoria, yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye kiwanja cha shule hiyo.

''Mimi nipo eneo la tukio ambapo bomba la maji limeporomoka, lakini mpaka sasa hivi mmoja amefariki na mwingine ni majeruhi na amewekwa ICU. Hii ni ajali ambayo imewapata watoto wawili nafikiri walikuwa wanayachezea yakaporomoka'', amesema Kamanda Mwakalukwa.

Kamanda Mwakalukwa amelitaja jina la mtoto aliyefariki kuwa ni Paul Moses Mlyambula, ambapo majeruhi wa ajali hiyo amelazwa katika Hospitali ya mkoa ya Kitete kwa ajili ya matibabu zaidi.
Chanzo - EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527