WAZIRI MKUU AMWAKILISHA RAIS MAGUFULI MKUTANO WA TICAD 7 ....ASEMA TANZANIA INAHITAJI TEKNOLOJIA YA UHAKIKA KUFANIKISHA UCHUMI WA VIWANDA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Tanzania inahitaji kuwa na teknolojia mpya na ya uhakika ili kufanikisha mkakati wa Seikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli wa kukuza uchumi na kufikia wa kati ifikapo 2015 kupitia sekta ya viwanda.


Ameyasema hayo leo (Jumatano, Agosti 28, 2019) katika Mkutano wa Saba wa Tokyo International Conference on African Development (TCAD 7) uliofunguliwa na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe kwenye ukumbi wa hoteli ya Pacifico Yokohama nchini Japan.

Waziri Mkuu ambaye amemwakilisha Rais Dkt. John Magufuli katika mkutano huo amesema kwamba ujenzi na uendeshaji wa uchumi wa viwanda   unahitaji sana teknolojia kutoka  ndani na nje ya nchi.

Amesema ujezi  wa uchumi wa viwanda utajikita katika matumizi ya malighafi yanayopatikana nchini kama vile mazao ya kilimo, uvuvi, mifugo na madini kwani Tanzania imebarikiwa kuwa na ardhi nzuri na hali ya hewa  inayofaa kwa kilimo pamoja na kuwa mali asili nyingi.

Waziri Mkuu amesema hivi sasa Tanzania inaandaa miundombinu na huduma mbalimbali zitakazofanya uwekezaji katika sekta ya viwanda ufanyike katika mazingira yanayokidhi matarajio ya wawekezaji na wateja wao.

Ametoa mifano wa  ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Nyerere katika mto Rufiji, ujenzi wa Reli ya kisasa ya SGR , ujenzi wa barabara za lami, ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania na upanuzi wa Bandari za Dar es salaam, Mtwara na Tanga kuwa ni baadhi ya mipango ya Serikali ya kuifanya nchi iwe na sifa na viwango  katika suala la uwekezaji wa  viwanda.

“Utaratibu wa Blue Print ulioandaliwa na Serikali kwa lengo la  kuondoa kero mbalimbali katika uwekezaji na biashara nchini Tanzania ni mfano hai unaodhihirisha kamba Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kushirikiana na sekta binafsi kujenga uchumi wa viwanda.”

Awali,akifungua mkutano huo, Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe amesema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita,  uwekezaja uliofanywa  Barani Afrika na wawekezaji binafsi kutoka nchini Japan umefikia Dola za Marekani bilioni 20. Ameahidi kuwa uwekezaji huo utaendelea kuengezeka.

Viongozi mbali mbali kutoa nchi za Afrika wamehudhuria mkutano huo akiwemo Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Rais Uganda, Yoweri Musseveni pamoja na Waziri Mkuu wa Mauritius, Pravini Kumar.

Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi  na viongozi mbalimbali kutoka Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,        
JUMATANO, AGOSTI 28, 2019.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527