WAZIRI MKUU AAGIZA SAME SEKONDARI IPEWE GARI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Bi. Anna-Clare Shija apeleke gari haraka katika shule ya sekondari ya wavulana ya bweni ya Same ili kumsaidia mwalimu mkuu endapo kutatokea dharura.

“Shule hii ina wanafunzi zaidi ya 800 lazima iwe na chombo cha usafiri kitakachotumika kwa dharura za kuwapeleka hospitali wanafunzi pale wanapougua. Sasa hivi mwanafuzi akiugua, Mwalimu Mkuu anafanyaje? Ni kama ameachiwa jukumu hili peke yake,” alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Ijumaa, Julai 19, 2019) wakati alipotembelea shule hiyo na kuzindua mradi wa ukarabati wa shule kongwe ya sekondari ya Same na kisha kuzungumza na wanafunzi, walimu na baadhi ya wazazi waliokuwepo.

Waziri Mkuu alimwita Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Bi. Shija na kumtaka atoe jibu hadharani kwamba ni lini atapeleka gari hilo shuleni hapo. Mkurugenzi huyo aliahidi kulipeleka gari hilo ifikapo Jumatatu jioni (Julai 22, 2019).

“Haya maelekezo ni kwa wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wenye shule ambazo zina wanafunzi zaidi ya 700. Mnapaswa kuhakikisha kunakuwa na gari la shule ili ikitokea dharura, Mkuu wa Shule aweze kuingilia kati na kupata ufumbuzi.”

“Wakurugenzi mnatakiwa kutambua shule hizi ni zenu, kwa hiyo mnalo jukumu la kuzihudumia. Shule hii ya Same ina wanafunzi zaidi ya 800 na wanalala hapa hapa, ni lazima kuwe na gari la kuwahudumia hasa wakati wa dharura.”

Pia amemuagiza Mkurugenzi huyo atafute daktari na muuguzi mmoja na awapangie kwenye shule hiyo ili waweze kutoka huduma kwa wanafunzi na kuwapunguzia adha ya kwenda mjini kutafuta huduma hiyo.

Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo baada ya kupokea changamoto zilizowasilishwa na kijana Omary Said wa kidato cha sita mchepuo wa PCB ambaye alisema shule hiyo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji; uchakavu wa mabweni; ukosefu wa zahanati ya shule na uhaba wa walimu wa sayansi hasa wa masomo ya fizikia.

Mapema, akitoa taarifa ya ukarabati, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bw. Hoza Mgonja alisema ukarabati huo ambao umegharimu sh. milioni 919, ulifanikisha ukarabati wa majengo saba ya madarasa yenye vyumba 22; maabara tatu, vyoo viwili vyenye matundu tisa; jengo moja la walimu; maktaba yenye vyumba viwili na ofisi mbili; vyoo viwili vyenye matundu manne na miundombinu ya umeme na majitaka.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake mkoani Kilimanjaro kwa kutembelea wilaya ya Mwanga ambako atazungumza na watumishi na kisha ataenda kijiji cha Kirya, Nyumba ya Mungu kukagua mradi wa maji wa Same - Mwanga - Korogwe.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527