WAZIRI KAMWELWE AZINDUA TRENI YA MAJARIBIO SGR

Na Grace Semfuko,MAELEZO.
Serikali imeanza mchakato wa ununuzi wa vichwa 22 vya treni, mabehewa 1,430 ya mizigo na Mabehewa 60 ya Abiria vitakavyotumika kwenye uendeshaji wa Reli ya kisasa ya SGR ambayo ujenzi wake unaendelea.


Yapi Merkez inajenga Reli ya SGR awamu ya kwanza kutoka Dar Es Salaam hadi Morogoro ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 56 na awamu ya pili kutoka Morogoro hadi Makutupora Mkoani Singida ikiwa imefikia asilimia 52 zote zikiwa na urefu wa zaidi ya kilomita 722 na zinajengwa kwa gharama ya fedha za ndani shilingi Trilioni 7.2.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe wakati akizindua Safari ya kwanza ya majaribio ya Treni ya Wahandisi kwenye eneo la Soga lililopo Kibaha Mkoani Pwani.

Injinia Kamwelwe alisema mpango wa sasa wa Serikali ni kuwa na Seti tano za Treni  za SGR zitakazokuwa na behewa nane za abiria, mpango ambao unalenga kuimarisha  sekta ya usafirishaji wa reli.

“Ndugu zangu Watanzania, leo hii tumezindua majaribio ya njia ya reli yetu, hii inamaana kwamba tupo katika mipango ya kuhakikisha reli inakamilika kwa wakati, tumetembea kilomita 20 za majaribiop, reli ni salama kabisa, haina kikwazo,sasa tumeanza mchakato wa kununua vichwa vya treni 22 na mabehewa yake 60 ya Abiria na 1,430 ya Mizigo” alisema Waziri Kamwelwe.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania TRC Masanja Kadogosa amesema zoezi la majaribio ya awali ya treni ya wahandisi ni hatua muhimu ya kuhakikisha reli hiyo inapitika bila kikwazo kwani inakagua na kuimarisha miundombinu ya reli hiyo.

Alisema zoezi hilo la awali limekuja kufuatia kukamilika kwa baadhi ya maeneo ya kupita treni kuanzia Soga Wilayani Kibaha Mkoani Pwani, kuelekea Morogoro na kuongeza kuwa treni rasmi kwa ajili ya kupita reli hiyo itawasili hivi karibuni.

Zoezi la majaribio ya uendeshaji wa Reli ya kihandisi ulishuhudiwa na Waziri Kamwelwe, Maafisa wa Shirika la Reli Tanzania TRC pamoja na Waandishi wa Habari ambao walitembea na treni hiyo kwa kilomita 20. 

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527