WAZIRI JAFO AAGIZA HOSPITALI YA UHURU IKAMILIKE NDANI YA MEZI 6 ILIYOPANGWA.


Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Mhe Suleiman Jafo amefanya ziara maalum ya kukagua ujenzi wa Hospital ya Uhuru inayojengwa kwa maelekezo ya Mhe Rais Dk John Magufuli katika Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma ambapo ameagiza ujenzi wa Hospitali hiyo ukamilike ndani ya miezi 6 iliyopangwa..

Waziri Jafo ametoa Maelekezo hayo kwa   Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi(SUMA JKT) linalojenga hospitali ya Uhuru iliyopo wilayani Chamwino mkoani Dodoma kuhakikisha inakamilisha ujenzi huo ndani ya miezi sita kama walivyokubaliana.

Hospitali hiyo inajengwa baada ya Rais Magufuli kuelekeza kufanya hivyo katika sherehe za Uhuru mwaka 2018 ambapo alifuta sherehe hizo na kupeleka Fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe hizo kujenga Hospitali mkoani Dodoma.

" Nishukuru leo kwa kufanya ziara hii maalumu ya kukagua ujenzi wa Hospitali hii ambayo ni malekezo kutoka kwa Mhe Rais, lakini pia hata hivyo baada ya gawio la Serikali kutoka Kampuni ya Airtel Mhe Rais alielekeza Fedha hizo kuletwa kwenye mradi wa ujenzi wa Hospitali hii ya Uhuru.

"  Na kama mnavyokumbuka nilikuja siku za nyuma Juni 19 kukagua lakini sikuridhishwa baada ya kukuta ujenzi haujaanza ndio maana nimetoa maelekezo kwamba ujenzi uanze mara moja kwa kutumia vikosi vya Jeshi ili kutimiza azma ya Mhe Rais katika kutoa huduma za Afya kwa wananchi, na tayari wenzetu wa Suma JKT wameshaanza kazi hii," amesema Mhe Jafo.

Amesema tayari eneo lote la Ekari 40 limeshasafishwa ikiwemo kujenga uzio pamoja na ofisi kuleta vifaa vya ujenzi huku pia akieleza kwamba TBA wataendelea kusimamia suala la ramani na kutoa ushauri wa mradi huo na wataendelea kutumia utaratibu wa 'false acount' kutokana na kuwapatia mafanikio katika kufanikisha kazi za Serikali za Mitaa.

" Kwa kweli leo nimeridhishwa na hatua ya awali ambayo tumefikia katika ujenzi wa Hospitali hii, na niwaombe wataalamu wangu kuacha kufanya kazi kwa mazoea na tunapotoa maagizo basi wayatekeleze kwa wakati, lakini ni matarijio yetu hadi kufikia Januari, 2020 tutakua tumeshamaliza ujenzi huu," amesema Mhe Jafo.

Kwa upande wake Mhandisi kutoka Wakala wa Majengo Tanzania TBA, Daniel Mwakasungura amesema Hospital hiyo ya Uhuru itakuwa ni ya Ngazi ya Wilaya ambapo kwa agizo la Mhe Rais awamu ya kwanza ni kujenga majengo ya wagonjwa wa nje ikiwemo huduma za maabara na Kliniki ya Mama na Mtoto.

" Hela iliyotengwa ambayo Tumeingia mkataba na Suma JKT ni Shilingi Bilioni 3 ambazo zitajenga hivyo nilivyovitaja na tunatarajia kukamilisha mradi huu baada ya miezi sita kama ambavyo tuliekezwa," amesema Mwakasungura.

 Kwa Upande wake,  Mhandisi wa Suma JKT, Luteni Kanali Onesmo Njau amesema walikabidhiwa jukumu la ujenzi huo Juni 19 mwaka huu na tayari washatekeleza maelekezo kutoka kwa Mhe Jafo ikiwemo kuandaa ofisi, sehemu za kuishi kwa watendaji na muda sio mrefu wataanza ujenzi ili kukamilisha mapema kama ilivyoelekezwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527