MWAKYEMBE : WATANZANIA WAMEKUWA NA MWAMKO MKUBWA KATIKA MICHEZO


Na Shamimu Nyaki –WHUSM
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe ametoa pongezi kwa watanzania kwa kuwa na mwamko mkubwa wa kupenda michezo kuanzia kushiriki,kushangilia pamoja na uhamasishaji ambao umechangia kwa kiasi kikubwa  mafanikio na  maendeleo ya michezo hapa nchini na uwakilishi mzuri nje ya nchi. 


Dkt.Mwakyembe ameyasema hayo leo Jijini Dodoma alipokuwa anamuwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluh Hassan katika mashindano ya riadha ya Capital City Marathon ambapo amesema kuwa kwa sasa nchi yetu imeanza kurudi katika ramani ya michezo kutokana na watanzania kushriki kwa wingi katika michezo mbalimbali. 


“Nawapongeza sana Watanzania wamekuwa na ari kubwa sana ya kushirikiki michezo hasa riadha ambayo imetutangaza vyema nje ya nchi,ni matuamini yangu mtaendelea kufanya vizuri zaidi lakini pia na michezo mingine vijana endeleeni kuchezakwa bidii zaidi  kwakua michezo sasa ni chanzo kikubwa cha kipato”amesema Dkt.Mwakyembe. 


Aidha Dkt.Mwakyembe ameongeza kuwa Taifa limekuwa na uwakilishi mzuri katika mchezo wa Soka kwani limepata nafasi ya kushiriki AFCON 2019,kuongezeka kwa timu zitakazoshiriki Klabu Bingwa Afrika ambayo ni Simba na Yanga pamoja na Klabu Mbili zitakazoshiriki Kombe la Shirikisho ambazo ni Azam FC na KMC. 


Katika hatua nyingine Mhe.Waziri Mwakyembe ameiagiza Idara ya Maendeleo ya Michezo kushirikiana na wadau kuwa na utaratibu wa kuandaa orodha ya wadhamini  wanaojitokeza na namna wanavyodhamini mashindano mbalimbali ili kuweka kumbukumbuku vizuri na kutoa ushauri panapowezekana katika kuimarisha Sekta hiyo. 


Kwa upande wake Mratibu wa Mbio hizo Bw.Nsolo Mlozi mbali na kuishukuru Serikali kwa ushirikiano iliyotoa pamoja na washiriki waliojitokeza  ameishauri jamii kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi na kushiriki mashindano mbalimbali ya riadha ili kujenga miili yao kwa kuimarisha afya lakini pia kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ambayo kwa sasa yamekuwa yakiwatesa wananchi wengi. 


Vilevile Bw.Nsolo ameongeza kuwa Capital City Marathon ilianza na kuwa na idadi ndogo ya washiriki  lakini mwaka huu idadi imeongezeka na kufikia washiriki 2,200 ambao kulingana na miundombinu imara ya Jiji la Dodoma wameweza kukimbia bila kupata changamoto yoyote.


Naye mshindi wa km 21 kwa upande wa wanaume  Bw.Emmanuel Giniki amesema kuwa mchezo wa riadha ni mchezo ambao unahitaji kuwa na mazoezi ya mara kwa mara ili kuweza kufanya vizuri ambapo amewashauri vijana wengi kujitokeza katika mashindano mbalimbali ya riadha yanayotokea ili kupata kipato pamoja na kupata ajira. 


Mbio za Capital City Marathon zinafanyika kwa mara ya pili Jijini Dodoma ambapo mwaka huu zimehusisha mbio za KM 22 Baiskeli,km.21wanawake na wanaume,km 10 wanawake na wanaume pamoja na km 5.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527