OJADACT YATOA TAMKO KUHUSU MSANII IRENE UWOYA KUDHIHAKI PESA YA TANZANIA NA WAANDISHI WA HABARI


Taarifa  kwa waandishi wa  habari,

Ndugu  Waandishi wa  habari   Chama  cha  Waandishi wa  Habari wa Kupiga  Vita Matumizi  ya  Dawa  za Kulevya  na Uhalifu Tanzania  OJADACT kinalaani  kitendo  kilichofanywa  na  Msanii  Irene  Uwoya  cha  kudhihaki    fedha  yetu  na  kuwadhihaki  Waandishi wa  habari  kwa  kuwarushia  fedha.


Msanii Irene Uwoya alionekana  kupitia   clip   ya  Video iliyosambaa  akiwarushia fedha waandishi wa habari na baadhi  ya waandishi  waliokuwepo kwenye  mkutano huo walipigana  vikumbo  kugombania  fedha zilizorushwa na  msanii  huyo.

Tukio  hilo  lilitokea   Julai  15:07:2019  Jijini  Dar es Salaam wakati  Irene   Uwoya akizungumzia juu ya  uzinduzi wa urushaji wa filamu kampuni ya swahili inflix.

Kitendo  hicho  ni  kitendo  cha  dhihaka  kwa  waandishi wa  habari  na  hakina  sababu  ya  kufumbiwa  macho  zaidi  ya  kukemewa  na  kila  mtanzania , kwani  ni  kitendo  kinachobeba  tafsiri  ya  dhihaka  ndani  yake  na  pia  kwenda  kinyume  na sheria  za  Nchi. OJADACT, tunapiga   Vita  uhalifu   huu  kwetu  ni  uhalifu  wa  kuvunja   sheria  za nchi.

Kwa mujibu wa sheria ya benki ya Tanzania  ya mwaka 2006, kifungu cha 26 benki kuu ndiyo yenye mamlaka juu ya fedha Nchini na sio Uwoya  ambaye  aliamua  kudhihaki    fedha   kwa  kuwarushia  Waandishi wa  habari.

Pia Sheria ya fedha inakataza mtu kudhihaki fedha, hivyo anapaswa akamatwe na ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria hizo.  

Ndugu  Waandishi wa habari  mtambue  kuwa, fedha ni moja ya alama  ya Taifa, hivyo ni kosa la jinai  kudhihaki na kukejeli sarafu au noti  kama   alivyofanya Msanii   Uwoya kitendo  hicho  ni kwenda  kinyume na sheria za nchi.

Yapo  matukio  ya  nyuma  yanayofanana  na hili,  mfano  ni  tukio  la  msanii  Maua Sama ambaye  alidhihaki    fedha  na kuchukuliwa  hatua  stahiki  na  vyombo  vya  Ulinzi  na Usalama,   Pia   Benki  kuu (BOT) ilitoa  waraka  wa  kuwambusha  watanzania  kutodhihaki  fedha  kwani  ni kinyume  cha  sheria.

Kwa  upande wa waandishi   nao   waliyatupa pembeni  maadili   ya  taaluma  yao  na kukubali kuidhalilisha taaluma ya habari kwa kujua wazi kuwa, kilichokuwa kinafanywa na Owoya   sio  sahihi,  hivyo  OJADACT  tumesikitishwa  na mwitiko wa Baadhi  ya  Waandishi  hao na kuvunja maadili ya  kitaaluma.


MAPENDEKEZO

·         OJADACT   tunaitaka    Wizara ya  Habari,  Utamaduni, Sanaa na Michezo  kupitia kwa  Waziri  mwenye  dhamana  Harrison  Mwakyembe kumchukulia  hatua   msanii   Irene  Uwoya  mara  moja ili  iwe  funzo  kwa  jamii.

·         Wahariri  wa  vyombo   vya  habari  husika   vilivyotuma  waandishi kwenye  mkutano  huo  vifanye  mapitio ya video  iliyokuwa  ikisambaa  kuwabaini  waandishi  waliohusika  na kuwapa  onyo  kali  juu  ya  vitendo  vyao  vya  kuidhalilisha   taaluma   ya  habari

·         Taasisi  za kihabari  ziongeze  warsha  za  uchechemuzi  kwenye   vipengele  vya  maadili  ya  uwandishi wa habari

·         Wadau  wa  habari  wenye nia  njema  ya  kufanya  kazi  na  vyombo  vya  habari  watoe  mialiko  kwa kutumia  taasisi  na  sio  mwandishi  mmoja mmoja   ili  kusaidia  kuthibiti  utovu  wa kimaadili  kwa waandishi

·         Wizara  iwape  mafunzo  maalumu  kundi  la  wasanii  ili wazijue  sheria  za Nchi kwani  inaonekana ni changamoto  kwao  kwenye kujua  sheria.


WITO:

OJADACT  tunatoa  wito  kwa Watanzania  kuzijua sheria  na  kuzielewa  ili kuepuka  kuvunja  sheria  za  Nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527