UINGEREZA YAPENDEKEZA JESHI LA ULAYA KATIKA GHUBA YA UAJEMI


Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema uwepo wa vikosi vya kigeni katika eneo hilo hautasaidia chochote bali hatua hiyo itasababisha mvutano. Rais Rouhani, ameongeza kusema kuwa Iran na Oman ndio zenye jukumu la msingi la kulinda eneo muhimu la pwani ya Hormuz.

Iran pia imesisitiza kuwa hali mbaya na mivutano ya sasa katika Mashariki ya Kati inatokana na kujiondoa kwa Marekani katika mpango wa nyuklia wa mwaka 2015 (JCPOA), uliofikiwa kati ya Iran na mataifa yenye nguvu.

Uingereza ilisema Jumatatu kuwa inajiandaa kuzindua kikosi kitakachoongozwa na nchi za Ulaya kujibu hatua ya Iran ya kuikamata meli ya mafuta iliyokuwa na bendera ya Uingereza mnamo Julai 19.

Kikosi maalum cha kijeshi cha Iran (IRGC) kiliikamata meli iitwayo Stena Impero katika bahari ya Hormuz baada ya kudai kwamba meli hiyo ilikaidi kujibu wito wa dharura na kuzima mawasiliano yake ya radio baada ya kuigonga mashua ya uvuvi.

Serikali ya Uingereza imekosolewa kwamba haikuchukua hatua madhubuti ya kulinda meli zake.

Ni wiki mbili sasa tangu kukamatwa meli ya Uingereza – ‘'Stena Impero'' ambapo hali hiyo imejitokeza baada ya kikosi cha wanamaji wa Uingereza kuitia nguvuni meli ya Iran ‘'Grace 1'' katika pwani ya Gibraltar kwa madai kwamba ilikuwa inasafirisha mafuta kwenda Syria hatua ambayo inakiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya.

Merikani imesema itaongeza uwepo wa majeshi yake katika eneo hilo ili kufuatilia shughuli za Iran. Lakini Iran imesema inaamini nchi za Mashariki ya Kati ndio zinapaswa kuhakikisha usalama wa meli zinazopita kwenye bahari ya Hormuz.

Mahusiano kati ya Iran na Marekani yanayumba tangu Rais Donald Trump aachane na mpango wa nyuklia wa mwaka 2015 na kuiwekea tena Iran vikwazo kwenye shughuli za usafirishaji wake wa mafuta.

Siku ya Jumapili, Wolfgang Ischinger, balozi wa zamani wa Ujerumani nchini Marekani ambaye sasa ni mkuu wa Mkutano wa Usalama wa Munich, amesema anataka jeshi la Ujerumani lihusike zaidi kwenye eneo la Ghuba. 

Ischinger amesema Ujerumani haifai kuangalia yanayotokea kutoka pemben na hasa ikiwa nchi zingine zinajadili kuhusu kuunda kikosi kujihami katika Ghuba.

Serikali ya Ujerumani bado haijaamua iwapo itashiriki. Waziri wa Ulinzi Annegret Kramp-Karrenbauer ametoa maoni kwamba Ujerumani inaweza kushiriki katika kuundwa kikosi cha jeshi kilichopendekezwa na Uingereza. 

Waziri wa Mambo ya nje Heiko Maas amesema hata hivyo mipango hiyo bado ipo kwenye hatua za mwanzoni.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527