TAMASHA LA ZIFF 2019 LAFUNGULIWA RASMI,FILAMU YA SUBIRA KUTOKA KENYA GUMZO



Na Andrew Chale, Zanzibar

TAMASHA la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF) la 22 kwa mwaka huu limefunguliwa  rasmi jana jioni mjini hapa huku likishuhudiwa na umati mkubwa kutoka sehemu mbalimbali akiwemo mgeni maalum mwanamuziki mkongwe wa Afrika Kusini, Mwimbaji wa wimbo wa Zanzibar, Sipho Mabuse.


Katika ufunguzi huo, filamu ya Subira kutoka Kenya ndio ilikuwa filamu ya ufunguzi mwaka huu ambapo iliteka hisia za watu walifika kulishuhudia tamasha hilo.

Filamu hiyo ya Subira iliyotengenezwa kisiwa cha Lamu nchini Kenya imejaa visa na mikasa ya binti mdogo Subira kwa mzazi wake kutaka kumuozesha iliaondoke nyumbani.

Awali mgeni rasmi wa ufunguzi wa tamasha hilo, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto,  Maudline Cyrus Castico aliyemwakilisha Asha Balozi Idd Mke wa makamo  wa pili wa Rais wa Zanzibar , alipongeza juhudi za  ZIFF  kwa kukuza vipaji vya Watanzania kupitia  filamu.

Waziri Castico aliwataka wananchi wa Zanzibar  kuchangamkia fursa zinazotokana na ZIFF ikiwemo mafunzo ya uandaaji wa filamu na mambo mbalimbali ikiwemo uwepo wa wageni  wanaofika katika msimu wa tamasha hilo.

“Nawapongeza ZIFF kwa kufikisha umri wa miaka 22, lakini pia naendelea kutoa wito kwa wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kulidhamini tamasha hili kwani  uwepo wake ni kielelezo cha ukuaji wa uchumi.” Alisema Bi. Castico.

Aidha, Bi. Castico alipongeza programu za watoto ambazo zinaendeshwa sambamba na ZIFF kuwa zitawajenga watoto katika uelewa mpana kwenye ukuaji wa vipaji vyao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF, ambaye ni Waziri wa Habari, Utalii na mambo ya Kale, Mahmoud  Thabit  Kombo aliendelea kutoa wito kwa wadau wakiwemo wafanyabiashara na taasisi binafsi za za kiserikali kujitokeza kwa wingi kudhamini tamasha hilo kwani ni moja ya matamasha makubwa ya filamu katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Nampongeza  Mzee Saidi Salim Bakhresa kwa udhamini mkubwa kwenye tamasha letu mwaka huu kupitia Azam Media.

Tunaomba na wadau wengine kujitokeza kwa wingi kwani uwepo wa tamasha visiwani hapa ndio ukuaji wa  uchumi wetu kwa pamoja” alieleza Mahmoud Thabit Kombo.

Kwa upande wao viongozi wakuu wa ZIFF akiwemo Mkurugenzi Mtendaji Faith Isakpere na Mkurugenzi wa tamasha hilo, Bi. Firdouse Bulbulia  waliwashukuru watu wote kwa kuliunga mkono tamasha hilo huku wakisisitiza kukuza utamaduni wa mwafrika.

Akizungumza , Bi Firdouse Bulbulia alibainisha kuwa, ZIFF ni miongoni mwa tamasha kubwa la filamu barani Afrika likiwa la tatu hivyo watu waendelee kuliunga mkono  kwa kukuza utamaduni wa mwafrika na zaidi kupenda vya Afrika.

Mdhamini mkuu wa tamasha hilo kwa mwaka huu ni Azam Media kupitia azam tv.
Pia wadhamini wengine ni  Zanlink, Global Education link, Zenjy water, Park  Hyatt, Maru maru hotel, Zancinema, Print Plus, Memory of Zanzibar, SOS Villages  na wengine wengi.

Tamasha hilo limeanza Julai 6- na kutarajiwa kufikia tamati Julai 14 mwaka huu.

filamu 208 zinaonyeshwa kwenye tamasha hilo mbapo filamu 33 miongoni mwa hizo zinatoka Tanzania, kati yake 14 Visiwani Zanzibar na 19 Tanzania Bara.


Filamu hizo zote zinaoneshwa bure kwa watu wote katika kumbi  za Ngome Kongwe,  Zancine na Beach House.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post