NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII AIAGIZA TANAPA KUPITIA UPYA SHERIA YA TOZO YA KIINGILIO KWA WATALII WANAPOTOKA NJE YA HIFADHI


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu ameiagiza Hifadhi za Taifa ( TANAPA) kupitia upya sheria ya tozo ya kiingilio kwa watalii wanapotoka nje ya Hifadhi  inayowalazimu kulipwa tena wanapoingia ndani ya Hifadhi maarufu kwa jina la Single Entry waiondoe kwenye maeneo yanayolalamikiwa kuwa imeua shughuli za Utalii kwenye  vijiji vinavyozunguka Hifadhi.

Aidha,Mhe. Kanyasu ameagiza TANAPA iangalie maeneo ambayo inadhani ni muhimu  kwa Single Entry iendelee kutumika  kuwa waweke mfumo wa kielektroniki wa utambuzi wa vidole ( Biometric Identity) utakaoweza kutumika kubaini udanganyifu endapo utafanyika.

Amesema mfumo huo utawalazimisha watalii kuweka kidole wakati wakiwa wanaingia na wakati wanapotoka nje ya Hifadhi.

Amesema hali hiyo itawasaidia Waongoza  watalii kutoka nje ya Hifadhi na Watalii wao kwa ajili kuzitembelea jamii zilizokaribu na Hifadhi na hivyo kuzisaidia jamii kunufaika moja kwa moja kupitia utalii wa kiutamaduni.

Hayo yamesemwa kupitia  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu wakati alipokuwa akifunga Maonesho ya 8 ya Utalii wa Utamaduni ya Serengeti mkoani Mara.

Amesema tangu kuanzishwa kwa Single Entry kumepelekea madhara makubwa kwa baadhi ya maeneo yaliyo karibu na Hifadhi za Taifa kudumaa  kiutalii.

Ameyataja  maeneo hayo yaliyokaribu na yaliyoathirika moja kwa moja kuwa ni ukanda wa Magharibi katika geti la Ndabaka katika Hifadhi ya Serengeti na katika  Hifadhi ya Ruaha.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa Maonesho hayo, Kanyasu amesema maeneo yaliyoathirika zaidi kutokana na kuwepo kwa Single Entry ni yale maeneo ambayo hayajapitiwa na barabara kuu pamoja na viwanja vya ndege.

Ametaja sababu zilizopelekea  kufa kiutalii maeneo hayo kuwa watalii walio wengi hulazimika kukaa ndani ya Hifadhi hadi muda wa masaa 24 yanavyoisha bila kutoka wakikwepa gharama endapo watatoka.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu alimueleza Naibu Waziri huyo  kuwa wilaya yake asilimia 80 ni eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti hivyo kutokana na uwepo wa Single entry wilaya hivyo imeathirika sana kwa vile imekosa watalii wanaotembelea vijijini tofauti na ilivyokuwa mwanzo kabla ya kuanzishwa.

" Mhe.Waziri tunakuomba uliangalie suala  hili, utalii wa kiutamaduni uliosaidia kuajiri wananchi wengi umekufa kutokana na Single Entry" alisisitiza

Ameongeza kuwa  endapo itaondolewa itasaidia watalii kuweza kutoka nje ya Hifadhi kuembelea vituo vingi vya utalii ambavyo vipo nje ya Hifadhi.

Naye, Anaeli Kilemi aliyesoma risala mbele ya Waziri huyo amesema Single entry imewadidimiza wananchi wengi ambao walikuwa wamejiajiri kupitia utalii wa kiutamaduni, Hivyo anaiomba serikali itatue tatizo hilo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527