MBUNGE ATOA ANGALIZO UUZAJI WA MAHINDI NJOMBE

Na Amiri kilagalila-Njombe

Mbunge wa jimbo la Wanging’ombe mkoani Njombe mhandisi Gelson Lwenge ametoa wito kwa wananchi mkoani humo kuacha kuuza kiholela mazao ya chakula hususani mahindi ili kuondokana na balaa la Njaa litakaloweza kutokea kutokana na uuzaji holela wa zao hilo.

Lwenge amesema mwaka jana soko la mazao hususani mahindi lilikuwa limeyumba ukilinganisha na mwaka huu hivyo baadhi ya wafanyabiashara nchini wamekuwa wakiongezeka mkoani Njombe kufuata mahindi.

Mbunge huyo ametoa wito huo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Lulanzi kilichopo Igima wilayani Wanging’ombe.

“Mwaka jana tumeyumba sana kwenye soko la mazao hasa mahindi lakini mwaka huu bei ni nzuri na inaendelea kupanda,maeneo mengine kwenye nchi hii hakuna mahindi ndio maana wote wanakimbilia Njombe, sasa nitoe angalizo tuwe waangalifu kwenye eneo la kuuza mahindi mwaka huu ili tusiwe na Njaa”alisema Lwenge

Kuhusu swala la Mbolea na pembejeo ambalo limelalamikiwa na wananchi wa kijiji hicho,Lwenge amesema serikali imejipanga kuleta bei ilekezi na naafuu badala ya kutoka kwa walanguzi ambapo walikuwa wakinufaika wachache.

Diwani wa kata ya Igima Paulina Samatta amesema zao la mahindi kwa kata hiyo limekuwa kubwa huku bei zikifikia shilingi 7000 kwa debe moja na kuungana na mbunge wa jimbo la Wanging’ombe kuhamasisha wananchi kuwa waangalifu katika biashara ya zao hilo la chakula.

“Mahindi katika kata yangu tumepata kwa wingi lakini bei pia zimefumuka,sasa hivi debe moja walanguzi wamepita wananunua mpaka shilingi 7000,na mimi ninahamasisha wananchi kutulia kwasababu kama tutauza mahindi yote tunaweza kuingia kwenye Njaa”alisema Samatta

Nao baadhi ya wananchi wa kijiji cha Lulanza akiwemo Fredy Kilasi na Blasto mpolya wamekiri kupanda bei kwa zao hilo na kuongezeka kwa wateja huku wakiahidi kutekeleza wito wa mbunge huyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527