KUNAMBI:UJIO WA DODOMA FOOTBALL CLUB SIMBA NA YANGA WATAISOMA NAMBA

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.

Halmashauri ya jiji la Dodoma  imeichukua na kuanza kuimiliki rasmi timu ya Dodoma Football  Club  ambayo ilikuwa inamilikiwa na wananchi hapo awali.

Akizungumza na waandishi wa Habari jana Julai 9,2019  katika hafla fupi ya kumtambulisha kocha mpya  atakayekinoa kikosi hicho,mkurugenzi wa jiji hilo Godwin Kunambi amesema timu  Dodoma FC   itakuwa na umuhimu mkubwa katika jiji hilo ambapo jiji la Dodoma lipo tayari kuihudumua na kuigharamikia timu hiyo.

Kunambi amesema”lengo  kubwa ni kuwatanabaisha WanaDodoma na Watanzania kwa ujumla kuwa jiji la Dodoma limeichukua rasmi na kuimiliki timu ya Dodoma FC  ili iweze kupaa  kimataifa zaidi,Mpira ni taaluma kama taaluma  zingine na hatutaingilia masuala ya ufundi katika timu itakuwa na bodi yake ya wataalam na washauri kuhusu Masuala ya Soka”

Aidha ,Kunambi ameongeza”Kuhusu kuimarishwa na kuanza kusimamiwa timu ya Dodoma FC   kufika hadi ligi  kuu  na si ligi kuu tu mpaka Simba na Yanga wataisoma Namba tayari tumeshampata kocha Mbwana Makata  kwa mkataba wa mwaka mmoja “Alisema.

Naye Kocha atakayekinoa kikosi hicho Mbwana Makata amesema atajitahidi katika kuhakikisha Dodoma FC inasonga mbele katika Mafanikio ya Soka.

“Nina imani kubwa tutakuwa na ushirikiano katika kukuza vipaji vya soka  jiji la Dodoma,Bajeti  ipo ,nimefundisha zaidi ya timu 20 nimepandisha vilabu vinne Twiga Sports,Mji Mpwapwa,Alliance na JKT Oljoro kikubwa ni Ushirikiano”alisema.

Katibu  wa  timu ya Dodoma FC Fourtnastus  Johson  amesema watahakikisha wanaisimamia vyema timu hiyo huku  Bakari Fundikila  Diwani wa Chang’ombe akizungumza kwa niaba ya Madiwani wa jiji hilo akisema uzalendo na ushirikiano ni nguzo muhimu katika kutekeleza majukumu.

Mbunge wa viti Maalum mkoa wa Dodoma Ester Bula amesema mchezo wa mpira wa Miguu unahitaji kuwa na kocha bora na wachezaji bora na ana mkakati wa kuanzisha timu ya  mpira wa Mguu ya wanawake  kwani kufanya hivyo inaweza kupatikana  vipaji ambao pia wanaweza kuchezea timu ya Taifa.

Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof.Davis Mwamfupe amesema jiji la Dodoma litakuwa kitovu cha wachezaji hivyo ni jambo la kila  mwanadodoma kuhakikisha anatoa Support  katika timu hiyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post