MNYETI : MKURUGENZI ATAKAYEKUJA NA HATI CHAFU,YENYE MASHAKA NI YAKE NA FAMILIA YAKE

Na Beatrice Mosses- Malunde1 blog Manyara.
Mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti amesema Mkurugenzi wa halmashauri yoyote ya mkoani Manyara atakayezalisha hati chafu au hati yenye mashaka hati hiyo  itakuwa ya kwake yeye na familia yake.


Kauli hiyo ameitoa wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani halmashauri ya wilaya ya Simanjiro cha kujadili na kujibu hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambapo aliipongeza halmashauri hiyo kwa kupata hata safi mfululizo.

“Mwenyekiti sisi katika vikao vyetu vya kiutendaji tumeshakubaliana kwamba  Mkurugenzi atakayekuja na hati chafu au hati yenye mashaka hiyo ni hati yake yeye pamoja na familia yake, sisi tunachotaka ni hati safi.

“Niwapongeze sana sisi kwenye mkoa huu tumebatika kupata wakurugenzi wasikivu kama ni changamoto ni ndogo ndogo ambazo kibinadamu tunaendelea kuzirekebisha wote kwa ujumla wako saba hakuna kichwa ngumu.

“Wapo wakurugenzi wengine wana vichwa vigumu kweli kweli hata umwambieje huwa hawasikii sasa  sisi huwa tunaambizana kwenye shida tunaelezana halafu mwisho wa siku tunasonga mbele”, Amesema Mnyeti.

Aidha Mnyeti amesema alifundishwa kitu kimoja na Wamaasai wa Arumeru kwa kuwa walikuwa ni wasikivu kwa asilimia 100 ukikaa na kuzungumza na wazee wa Kimaasai mkimaliza mmemaliza hawana maneno ya chinichini hivyo amewataka wana Simanjiro kukaa pamoja na kufanya kazi ili mwaka ujao wapate hati safi.

Hata hivyo amemwambia CAG aendelee kuwaambia madhaifu yao yako wapi wao wako tayari kujirekebisha kwani kukiri udhaifu ni njia mojawapo  ya kujiimarisha.

“Sisi  madhaifu yetu tutayakiri kwamba haya ni madhaifu na tutaenda kuyafanyia kazi na lengo letu mwakani tukiwa tunakutana hapa kusiwe na hoja hata moja iliyotoka kwako kwamba hii hoja imekaaje, ndo maana tukaomba hoja iliyokaa miaka kumi, nane, saba miaka mitano  uzifute kwa sababu zingine hatuna majibu nazo.

Naye Mkaguzi wa Nje mkoa wa Manyara Vitus Samwel amepongeza halmashauri zote za mkoani hapa kwa kupata hati safi kwani hiyo inaonyesha ni jinsi gani walivyofanya kazi kwa kushirikiana.

“Pamoja na kupata hati safi kwa halmashauri zote saba lakini nguvu za ziada zinatakiwa kuwekwa kwenye ukaguzi wa mwaka wa fedha 2018/2019 wa kuhakikisha taarifa zote zimeandaliwa kwa mujibu wa miongozo ya hesabu inayotakiwa kufuatwa”, Amesema Samwel.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527