WIZARA ZAANZA KUSHIRIKISHWA KUTOA MAONI KUHUSU MAPITIO YA SERA YA KILIMO


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Wizara mbalimbali zimeanza ushirikishwaji wa kujadiliana kuhusu utekelezaji wa Sera ya Kilimo ya Taifa ya Mwaka 2013 na kutoa maoni yao kuhusu mapendekezo ya kurekebisha Sera hiyo.


Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew John Mtigumwe ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha wadau kuhusu marekebisho ya sera ya Kilimo kinachofanyika Jijini Dodoma katika ukumbi wa Morena tarehe 13 Juni 2019.


Mhandisi Mtigumwe amesema kuwa Maboresho hayo yanalenga kuhuisha shughuli za kilimo ili ziendane na mahitaji halisi ya nchi ikiwa ni pamoja maendeleo ya viwanda.


Alisema, timu ya Wataalamu ya Wizara ya Kilimo inaendelea na ukusanyaji wa maoni kutoka kwa Wadau maeneo mbalimbali ya nchi ikizingatia pia ushiriki wa makundi mbalimbali ya Kijamii.


Katika kikao kazi hicho Mhandisi Mtigumwe alisema kuwa fursa hiyo ya kushirikishwa katika mchakato wa mapitio ya marekebisho ya Sera ya Kilimo, ni heshima kubwa kwa wadau hao. 

“Hivyo, nawasihi wadau wote mshiriki kikamilifu kutoa maoni yenu kwa uwazi na uhuru ili kuakisi uaminifu mliopewa na Wizara ya Kilimo. Aidha, maoni yenu ni muhimu katika maboresho ya Sera ya Kilimo yatakayochochea ukuaji wa sekta ya kilimo ambayo hutegemeana na sekta nyingine katika ukuaji wa uchumi kwa lengo la kufikia uchumi wa kati” Alikaririwa Mhandisi Mtigumwe


Kadhalika alisema pamoja na mambo mengine lakini wadau watapata fursa ya kutambua jitihada za Serikali zinazoendelea katika kurekebisha Sera ya Kilimo ya Mwaka 2013 na kutoa maoni yao kwa uwazi na uhuru katika marekebisho ya Sera yanayopendekezwa.


Aidha, Mhandisi Mtigumwe amesema kuwa pamoja na ukweli kwamba, Wizara imeandaa Rasimu ya Taarifa ya Utekelezaji wa Sera ya Kilimo ya Taifa ya Mwaka, 2013 pamoja na uchambuzi unaoainisha mapungufu ya awali (gap analysis). 


Hata hivyo, kikao hicho kitatoa mwanga zaidi wa mapungufu yaliyopo na kuyaainisha kabla ya kuendelea katika hatua zinazofuata.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post