WAZIRI MHAGAMA APOKEA MSAADA WA VIFAA SAIDIZI NA CHEREHANI KUTOKA UBALOZI WA CHINA

NA; Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amepokea cherehani na vifaa siadizi kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu vilivyotolewa na Ubalozi wa China nchini.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika ofisi ndogo za ubalozi huo zilizopo Jijini Dodoma, Waziri Mhagama alieleza kuwa Serikali inatambua haki za Watu wenye Ulemavu nchini hivyo imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki zao stahiki ikiwemo kuwapatia vifaa saidizi.

“Vifaa saidizi ni muhimu kwa kundi hilo maalumu kwa kuwa vinawawezesha kumudu mazingira yanayowazunguka na kuwasaidia kufanya shughuli zao za kila siku bila kukabiliana na changamoto,” alisema Mhe. Mhagama

Alieleza kuwa kutokana na vifaa hivyo kuwa ni ghali na upatikanaji wake umekuwa mgumu na kupelekea watu wenye ulemavu kushindwa kuvinunua, Serikali imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kununua vifaa hivyo.

Aliongeza kuwa, katika ujenzi wa uchumi wa viwanda Serikali kupitia Shirika la kuhudumia viwanda Vidogovidogo (SIDO) kushirikiana na wadau imejipanga kuimarisha utengeneza wa baadhi ya vifaa hivyo, vitakavyokuwa vinapatikana hapa nchini.

Aidha alitoa wito kwa jamii kubadili mtazamo na fikra potofu juu ya watu wenye ulemavu, bali watambue kundi hilo linaweza na linamchango mkubwa katika jamii na nchi kwa ujumla.

Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Bi. Wang Ke alisema kuwa Serikali ya China itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na Serikali ya Tanzania katika nyanja mbalimbali pamoja na kuendelea kutoa misaada kwa ajili ya wenye uhitaji.

Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa aliwataka wadau ndani na nje ya nchi kuendelea kujitokeza na kusaidia makundi yenye uhitaji maalumu, kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kusaidia masuala ya Watu wenye Ulemavu.

Katika hafla hiyo pia aliudhuria Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika masuala ya Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mhe. Fatma Toufiq na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza Mhe. Kemilembe Lwota.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527