WAZIRI LUGOLA AFANYA ZIARA UWANJA MPYA WA NDEGE JNIA


Na Felix Mwagara
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amefanya ziara katika Uwanja  wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal III) ya kuvikagua vyombo vyake vinavyotarajiwa kutoa huduma katika uwanja huo hivi karibuni.


Waziri Lugola aliwasili katika uwanja huo akiwa ameambatana na Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara yake, pamoja na taasisi zake, ambapo walipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA).


Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi uwanjani hapo, Waziri Lugola alisema hana shaka na utoaji wa huduma wa vyombo vyake katika uwanja huo mpya, kwa kuwa ameridhika na mipango ya utoaji huduma wenye weledi baada ya uwanja huo kufunguliwa.


“Wizara yangu ni wadau wakubwa katika utoaji huduma katika uwanja huu wa ndege, ni lazima nijue Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Idara ya Uhamiaji, wamejipangaje katika kutoa huduma bora kabisa hapa uwanjani, sina shaka nao nimeridhika baada ya kumaliza ukaguzi,” alisema Lugola.


Pia Waziri Lugola, alimuhakikishia Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Injinia Julius Ndyamukama, kuwa ameridhishwa na mpangokazi wa vikosi hivyo kwa namna viulivyojipanga kutoa huduma katika uwanja huo mpya.


“Nimeridhishwa na utendaji kazi wa Vyombo vya ulinzi na Usalama vilivyopo chini ya Wizara yangu kwa namna vilivyojipanga juu ya utendaji kazi na jinsi watakavyotoa huduma kwa wasafiri wa uwanja huu, ila nimepewa baadhi ya changamoto chache na tunaahidi kuzifanyia kazi mapema kabla ya uwanja huu kufunguliwa,” alisema Lugola. 


Lugola alihakikishiwa na viongozi wa majeshi hayo kuwa, watafanya kazi kwa nguvu zote kwa kutoa huduma bora katika uwanja huo.


 “Tupo tayari kuutumikia umma na kwa kuwa kazi zetu ni kuusaidia umma wa watanzania tupo tayari kuhakikisha uwanja huu mpya pamoja na viwanja vyote vinakuwa salama muda wote.”  Alisema Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt Anna Makakala. 


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Injinia Julius Ndyamukama, alimshukuru Waziri huyo pamoja na viongozi wa Wizara kwa kufika uwanjani hapo kufanya ukaguzi, ila alimuomba waziri huyo magari ya zimamoto yaongezwe ili kuhudumia uwanja huo mpya.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527