WATUMISHI WANAOTARAJIA KUSTAAFU WAASWA KUZINGATIA MABADILIKO YA MAISHA


Na Mwandishi Wetu
 Watumishi wanaotarajia kustaafu wameaswa kuzingatia mabadiliko ya maisha kutoka katika utumishi wa umma kwenda katika mfumo wa maisha ya  kawaida na kujiepusha kufanya miradi ambayo hawana ujuzi wa kutosha kuihusu. 


 Akizungumza katika mafunzo kwa yakuwajengea uwezo watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wanaotarajia kustaafu hivi karibuni ili wawe na mbinu za kuendana na mazingira hayo, Katibu Mkuuu wa Ofisi hiyo anayeshughulikia (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Doroth Mwaluko amesem kuwa Ofisi hiyo inatambua umuhimu wa wastaafu na faida za kujiandaa kustaafu. 


“ Kuna umuhimu mkubwa wa kutambua kuwa suala la kustaafu ni la kila mmoa wetu na ni muhimu kujiandaa vyema na maisha mapya ambayo kimsingi yatakuwa tofauti na haya ya utumishi wa umma mliyo nayo  kwa sasa” Alisisitiza Mwaluko 


Akifafanua amesema kuwa kila mtumishi wa umma lazima atambue kuwa ni mstaafu matarajiwa hivyo kujiandaa kwake ni jambo  muhimu. 


Kwa upande wake Muwezeshaji Kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni Jijini Dar es Salaam Bw. Peter Seme amesema kuwa watumishi hao wanaotarajia kustaafu watajifunza mambo mengi yakuwawzesha kuendelea na maisha yao kama kawaidia hata baada ya kustaafu. 


Alitaja baadhi ya mada kuwa ni pamoja na utayari wa kupokea mabadiliko baada ya kustaafu, Stadi za kuongeza kipato, Mtindo wa maisha bora baada ya kustaafu, Namna ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza baada ya kustaafu. 


Kwa upande wake mmoja wa watumishi hao  Bw. Esamo Sawaki amesema kuwa  wanaipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuandaa mafunzo hayo kwa ajili ya kuwajengea uwezo watumishi wa Ofisi hiyo ili waweze kukabiliana na changamaoto zinazoweza kujitokeza baada ya kustaafu. 


Aliongeza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kupata uzoefu kutoka kwa wastaafu wengine ambao tayari wana uzoefu katika kukabiliana na changamoto za kustaafu na hata kuelewa kazi ambazo ni za uzalishaji wanazoweza kuzifanya kama wastaafu ili kuwaletea tija. 


“Tutapata maarifa sahihi ya namna ya kutumia kiinua mgongo tutakachopewa baada ya kustaafu kutoka katika utumishi wa umma” Alisisitiza  Sawaki 


Mafunzo yakuwajengea uwezo watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wanaotarajia kustaafu hivi karibuni yanafanyika Jijini Dodoma kwa siku tano yakiwashirikisha watumishi hao kutoka kada mbalimbali.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527