SERIKALI YAIPATIA TUME YA MADINI NA KAMPUNI YA HUDUMA ZA MELI SHI. BIL. 17 KUBORESHA MAPATO


Na Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali, kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, imetoa Sh. billion 10.7, kwa Tume ya Madini nchini na Sh. billion 5.9, kwa Kampuni ya Huduma za Meli (Marine Service Company Limited -MSCL) kwa ajili ya kutekeleza Miradi  ya kimkakati, yenye lengo kuongeza mapato yanayotokana na madini pamoja na kuiwezesha Kampuni ya Huduma za Meli kujiendesha kibiashara.

Hafla ya utiaji saini mikataba ya fedha hizo umefanyika Jijini Dodoma kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Doto James na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt. Leonard Chamriho.

Bw. James alisema kuwa  Sekta ya Madini na Kampuni ya Huduma za Meli,  wajifunze kupitia miradi mingine ya kimkakati katika Halmashauri zilizopewa fedha, ili kuepuka changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwa baadhi ya Halmashauri kushindwa kufikia malengo.

“Fedha hizi sio za bure tutazifuatilia mpaka shilingi ya mwisho, ili kupata mrejesho wa kuchangia maduhuli katika Mfuko Mkuu wa Serikali, hivyo fedha hizo  zinatakiwa kutumika kwa ufanisi  kwa lengo lililo kusudiwa”, alisisitiza Bw. James.

Alisema Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imeunda kikosi kazi maalum ambacho kitakuwa kinafuatilia maendeleo ya miradi hiyo na kutoa taarifa Serikalini.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Pro. Simon Msanjila aliishukuru Serikali kwa kuwapatia fedha hizo na kuahidi kuwa watazitendea haki na kuongeza mapato ya Serikali.

"Tumepewa lengo la kukusanya maduhuli ya kiasi cha shilingi bilioni 475 katika mwaka huu wa fedha 2018/2019, nina kuhakikishia kuwa lengo hili tutalifikia kwasababu ya uwezeshaji huu wa Serikali na mwitikio mzuri wa wadau wa sekta ya madini katika kulipa kodi kwa hiari" alisema Prof. Msanjila

Alisema kuwa Sekta ya madini ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa nchi, uwezeshaji huo utawezesha kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiikumba Tume ya Madini kwa lengo la kuongeza ukusanyaji wa mapato yanayotokana na madini.

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kikula, alisema kuwa uwezeshaji huo utaiwezesha Tume hiyo kufikia lengo na kuahidi kuendelea na juhudi za kuhakikisha maduka ya madini nchini yanaboreshwa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt. Leonard Chamriho, aliishukuru Serikali kwa kuipatia Kampuni ya Meli nchini (MSCL) kiasi cha shilingi bilioni 5.9 zitakazotumika kukarabati baadhi ya meli  zilizopo pamoja na kuweka mifumo ya kieletroniki ya kukusanya maduhuli ya Serikali.

Aidha, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli, Bw. Eric Hamissi, aliahidi Serikali kuwa hawatoiangusha na kubainisha kuwa kampuni hiyo ni ya kimkakati na inaweza kuchangia uchumi wa nchi.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post