TAARIFA KWA UMMA KUTOKA MAKAO MAKUU YA JESHI LA POLISI NCHINI


Mtakumbuka kuwa Serikali ilitoa maelekezo kwa Taasisi zake  zinazohusika na ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali waanze kutumia mfumo wa malipo kwa njia ya kieletroniki yaani Government eletronic-Payment Gateway (GePG). 


Jeshi la Polisi nchini, katika kutekeleza maagizo hayo lilishaanza kupokea malipo kwa njia ya kieletroniki kwa malipo ya tozo ya makosa yanayotokana na madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani kwa kutumia mashine za POS. 

Katika kuendelea kutekeleza maagizo hayo ya Serikali ya kupokea malipo kwa njia ya kieletroniki ili kuhakikisha pia tunaendana na muda uliotolewa,  Jeshi la Polisi kuanzia tarehe 8/05/2019 lilianzisha  mfumo wa kukusanya malipo kwa ajili ya kulipia taarifa ya kupotelewa mali ( Loss Report) kwa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. 


Kwa sasa mfumo huu ambao unapatikana kwenye mtandao kupitia tovuti ya  https://lormis.tpf.go.tz  umeenea nchi nzima. Lormis ni kifupi cha Loss Management Information System.  Jeshi la Polisi limeanzisha tovuti hiyo ili kurahisisha huduma ya loss report kupitia mitandao ili kutekeleza maagizo ya Serikali kuwa ifikapo mwisho wa mwezi June, 2019 ukusanyaji wa maduhuli yote ya Serikali ufanyike kwa mfumo wa kieletroniki kupitia GePG. 

Mfumo huu ulioanzishwa na Jeshi la Polisi utamwezesha mwananchi kutoa taarifa za upotevu wa mali au nyaraka kwa kupitia mtandao na kuweza kupata loss report bila kufika Kituo cha Polisi, isipokuwa kwa anayetoa taarifa ya upotevu wa kitabu cha kumiliki silaha, kadi ya gari, hati ya kiwanja au shamba, huyu itamlazimu kufika kituo cha Polisi. Mwananchi anaweza kutoa taarifa ya kupotelewa mali au nyaraka kwa kutumia kompyuta au simu yenye internet.  

Taarifa hiyo inaweza kutolewa akiwa mahali popote pale ilimradi awe na kifaa cha kieletroniki chenye internet atakachotumia kutolea taarifa. Ili kutoa taarifa bila kufika kituoni inambidi mwananchi kutembelea tovuti ambayo nimeitaja awali ambayo ni https://lormis.tpf.go.tz inayopatikana kwa lugha ya Kiswahili na Kiingeleza. Akishaingia kwenye tovuti atabonyeza kitufe cha “ S a jili M a li I li y o p o t e a ” na ataendelea kujaza fomu  atakayoipata. Baada ya kujaza fomu hiyo atatakiwa kufanya malipo.   

Mfumo huu wa malipo wa Loss report unaowawezesha wananchi kulipa malipo hayo kupitia mfumo wa kieletroniki yaani Government electronic Payment Gateway (GePG) unapatikana kwenye mitandao yote ya simu na  kwenye mabenki.  Mwananchi anapojaza fomu ya Loss report kwenye mtandao atapata namba ya malipo (Control number) ambayo kupitia tovuti hiyo ya Polisi inaanzia na 99108 na kuendelea / kufuatiwa na namba nyingine. 


Endapo mwananchi ataamua kufanya malipo kupitia benki anachotakiwa ni kwenda  na  namba ya malipo (control number) na hapo  watamsaidia kufanya malipo. Kama mwananchi atatumia mitandao ya simu za mkononi atakapo andika kodi ya namba ya kufanyia miamala ya fedha ya kampuni ya simu, baada ya hapo atachagua namba 4(lipa bili), halafu  atachagua namba 5 (Malipo ya Serikali)na kisha ataingiza namba ya malipo (Control number) yake na kulipa kiasi cha Tsh 500/= 

Kwa wale wananchi waliopoteza laini za simu, kadi za benki  au vitambulisho na kujaza maombi yao kwa kutumia kadi zao za NIDA au namba ya NIDA  hawahitajiki kwenda Kituo cha Polisi kwani mfumo huu wa Loss report umeunganishwa na mfumo wa NIDA ambao una uwezo wa kuthibitisha  taarifa za vitambulisho hivyo moja kwa moja (online).Kwa maana hiyo mwananchi mwenye kitambulisho cha NIDA au namba na akawa amepoteza laini za simu ana uwezo wa kujaza fomu online na kupata loss report yake online.  


Kwa wale ambao watatumia vitambulisho vingine na kujaza fomu ya loss report watahitajika kufika Kituo cha Polisi ili kufanya uthibitisho. Kufika Kituo cha Polisi ni kwa sababu zifuatazo:- Moja ni ili Polisi waweze kuthibitisha kwamba aliyetoa taarifa ni yeye kutokana na kwamba kitambulisho alichotumia hakijaunganishwa na hakitumiwi na watoa huduma wengi kama cha NIDA.  

Aidha, wengine wanaotakiwa kufika kituoni ni wale waliopoteza mali zikiwemo  vitabu vya  kumiliki silaha, kadi za gari na hati za nyumba au mashamba hizi zinahitaji uchunguzi wa Polisi ufanyike kabla ya Loss Report haijatolewa kwa mhusika. Pia ambao wanatakiwa kuendelea kutoa taarifa zao katika vituo vya Polisi ni wale ambao hawana simu au kompyuta zenye internet itakayowezesha kutoa taarifa ya kupotelewa na mali au nyaraka kwa njia ya mtandao (online).   

Kwa wananchi wa aina hii Wakuu wa Vituo na Wahasibu wameshapata mafunzo na maelekezo ya namna ya kuwahudumia. Mfumo huu wa kulipia kwa ya njia ya mtandao (online) na kupata loss report kama nilivyosema tulianza na Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, napenda kuwajulisha kuwa mfumo huu unatumika kwa nchi nzima sasa. Hivyo ninapenda kuwapa taarifa watoa huduma za mawasiliano kuwa kuanzia sasa wawape huduma wananchi wote wanaofika kwao wakiwa na Loss report ya kieletroniki.    

Watoa huduma pale watakapokuwa na mashaka wanaweza kuthibitisha/ kuhakiki kama Loss report ya mwananchi ni halali au ya kugushi kwa kutumia njia mbili:- Njia ya kwanza ni kutembelea tovuti ya loss report ya Jeshi la Polisi ambayo ni https://lormis.tpf.go.tz na kwenda kwenye kitufe cha “Angalia Ripoti yako” hapo ataingiza namba ya malipo (Control Number) ambayo atapewa na mwananchi pamoja na namba ya kitambulisho chake,  ripoti ikitoka itakuwa ni sahihi na isipotoka itakuwa ni ya kughushi. 

 Njia ya pili,   kwa wale watoa huduma ambao wana mifumo ya kieletroniki na wangependa  kujiunga na mfumo huu tunatoa Application Program Interface      (API) ambayo itaweza kuwaunganisha na hapo wataweza kuwahakiki wateja wao kwa njia ya kieletroniki bila ya kufika au kutembelea tovuti yetu. 

Ili kupata hii API wawasiliane na Mkuu wa TEHAMA wa Jeshi la Polisi kwa barua pepe gabriel.mkungu@tpf.go.tz, au incharge wa Kitengo cha mifumo ya TEHAMA (godfrey.kapinga@tpf.go.tz). 


Jeshi la Polisi nchini linatoa wito kwa wananchi wote watumie mfumo huu kwani unaokoa muda na ni wa uhakika katika kufanya malipo ya Serikali kwa njia ya kieletroniki pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma ya loss report.

  Imetolewa na: David A. Misime - SACP

Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu ya Polisi. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post