SERIKALI YATANGAZA OPARESHENI MAALUMU NCHI NZIMA JUU YA MARUFUKU YA MIFUKO YA PLASTIKI

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.

Katibu mkuu wa Ofisi ya Makamu wa  Rais ,Mhandisi Joseph Malongo ametangaza operesheni   maalum ya Nchi nzima ya uzingatiaji wa Sheria ya usimamizi wa Mazingira juu ya marufuku ya Mifuko ya Plastiki  na Matumizi endelevu ya mifuko mbadala .

Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dodoma Mhandisi Malongo amesema kanuni za usimamizi wa Mazingira za kupiga marufuku mifuko ya Plastiki  za mwaka 2019 zimeanza kutekelezwa kuanzia tarehe Mosi ,Juni,2019 hivyo kwa mujibu wa kanuni hizo ,ni marufuku kuzalisha,kusambaza kuingiza nchini ama kusambaza nje ya nchi na kutumia Mifuko ya Plastiki iliyotajwa katika katazo hilo .

Mhandisi Malongo amebainisha ,kiwanda,kikundi cha watu au mtu binafsi atakayebainika  kukiukwa matakwa ya kanuni hizo atakuwa ametenda kosa la  jinai na hivyo sheria itachukua mkondo wake.

Hata hivyo,amesema baada ya kuanza kwa utekelezaji wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki,baadhi ya wazalishaji na wasambazaji wamebadilisha matumizi ya mifuko laini ya plastiki isiyokuwa na mishikio na kuitumia kama vibebeo vya bidhaa  kinyume na kanuni ya 8 ya kanuni za usimamizi wa Mazingira.

Mhandisi Malongo ameendelea kufafanua kuwa kanuni ya 9 inatoa Msamaha kwa baadhi ya vifungashio vya plastiki kwa ajili ya huduma za afya  au kwa vifungashio vinavyotumika kufungashia bidhaa za  viwandani ,sekta  za ujenzi ,sekta ya kilimo,vyakula au usafi na   udhibiti wa taka.

Shirika la viwango Tanzanzia TBS linaandaa   viwango vya vifungashio  ambavyo vitalazimisha kiwango cha unene,uwekwaji   lakiri na kutambulisha bidhaa iliyofungashwa kabla ya kuuzwa.

Katika kuhakikisha suala hilo linatekelezwa kwa  ufanisi zaidi,Mhandisi Malongo  amesema Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi  wa Mazingira nchini,[NEMC] linaendelea na Operesheni kabambe   nchi nzima ya kusaka  mifuko ambayo imebadilishiwa matumizi  yake na kukiuka sheria  ambapo operesheni hiyo itahusisha vyombo vya ulinzi  na usalama,kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya,mamlaka za  serikali za mitaa.

Vingine ni  mamlaka ya maabara ya mkemia  mkuu wa serikali,shirika la viwango Tanzania TBS,Mamlaka ya Chakula na Dawa ,TFDA,Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,Pamoja na mamlaka ya viwanja vya ndege,bandari ,Forodha,uhamiaji na usafiri wan chi kavu.

Ikumbukwe kuwa ni makosa kisheria kubadili matumizi ya vifungashio na kuwa mifuko ya kubebea bidhaa na adhabu stahiki zitatolewa  kwa watu watakaobadili matumizi ya vifungashio na kuwa vibebeo vya bidhaa huku Ofisi ya Makamu wa Rais ikiendelea kuelimisha umma  pia  ikisisitiza kutumia mifuko mbadala.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527