SERIKALI YA TANZANIA YAMUITA KAIMU BALOZI WA MAREKANI AJIELEZE KUHUSU TAARIFA YAO YA SHAMBULIZI LA KIGAIDI NCHINI


Tarehe 19 June 20, 2019, Ubalozi wa Marekani Nchini Tanzania ulitoa taarifa katika mitandao ya kijamii “Twitter” kuhusu angalizo la kiusalama “security alert”. Angalizo hilo la kiusalama lilitokana na uvumi unaodaiwa na ubalozi huo kusambaa kuhusu uwezekano wa kutokea kwa shambulio katika baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam.


Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulimwita katika ofisi ndogo za Wizara zilizopo Jijini Dar es Salaam, Kaimu Balozi wa Marekani Bi Ann Marie Warmenhoven – Tilias ili kutoa ufafanuzi wa “twitter” yao.

Ubalozi wa Marekani ulimtuma Mwakilishi wa Kaimu Balozi wa Marekani Bi Ann Marie Warmenhoven – Tilias kuonana na uongozi wa Wizara ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe. 

Bi Ann Marie Warmenhoven – Tilias ameutambua ujumbe huo na kukiri kuwa  umetumwa na ubalozi wa Marekani hapa nchini.

Katika ufafanuzi wake amekiri kuwa Ubalozi umefanya makosa ya kutoa tetesi ambazo hazikuwalenga raia wa Marekani pekee bali raia wote wakitambua kuwa Ubalozi hauna mamlaka ya kufanya hivyo jambo lililosababisha taharuki kwa wananchi na wageni wanaotarajia kuitembelea Tanzania.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeukumbusha Ubalozi wa Marekani umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi na taratibu za kidiplomasia zinazokubalika duniani kote katika utoaji wa taarifa za aina hii.

 Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe amewataka wananchi na Jumuiya za Kimataifa pamoja na wageni mbalimbali waliopo  nchini na wanaotarajia kuitembelea Tanzania kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwani mpaka sasa hakuna taarifa yeyote iliyothibitishwa ya kuwepo kwa tishio la aina hiyo hapa nchini na kwamba Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimejizatiti kukabiliana na matishio yeyote.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam.
20 Juni, 2019


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527