SERIKALI KUAJIRI WAKAGUZI WA NDANI 100


Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Josephat Kandege (Mb) amesema TAMISEMI imewasilisha maombi ya kupata kibali cha ajira ya Wakaguzi wa Ndani 100 ili kutatua changamoto ya uhaba wa watumishi wa Kada hii katika Sekretariet za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mhe. Kandege ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Kazi wa Wakaguzi wa Ndani unaofanyika kwa siku mbili katika chuo cha Mipango Jijini Dodoma.

Kandege amesema Wakaguzi wa Ndani ni watu muhimu, Serikali inawaamini na inatambua mchango wao  katika usimamizi wa fedha na Uwajibikaji hivyo ni vyema rasilimali watu ikawa ya kutosha ili kazi hii iweze kufanyika kwa ufanisi.

“Napenda mfahamu kuwa Wakaguzi wa Ndani ndio Jicho la Kwanza la Serikali bila  ninyi Serikali haiwezi kuona vitu ambavyo vinavyotokea kwenye matumizi ya Fedha; Mmekua mkituonyesha yale yote yanayotendeka kinyume na matumizi stahiki yaliyoelekezwa hivyo ajira hiyo itakwenda kutatua changamoto ya uhaba wa watumishi wa kada hii” Alisema Kandege.

Akizungumzia changamoto ya Ufinyu wa bajeti kwa vitengo vya ukaguziamesema  Serikali imeongeza bajeti za vitengo vya ukaguzi kutokaa shilingi 5.6 bilioni kwa mwaka wa fedha 2018/2019 hadi kufikia shilingi 6.4 bilioni kwa mwaka wa fedha 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 14.3.

“Ili kuleta tija na matokeo tarajiwa katika vitengo hivi Serikali itaendelea kuongeza bajeti ya rasilimali fedha ili muweze kujitegemea katika kutimiza majukumu yenu badala ya kutegemea fedha kwa wakaguliwa” Alisema Kandege.

Wakati huo huo Mhe. Kandege ameagiza Vitengo vya Ukaguzi wa Ndani kuhakikisha mianya yote ya ubadhilifu inabainishwa na kudhibitiwa kwenye mifumo ya kukusanyia mapato na usimamizi wa fedha.

Pia aliziagiza Halmashauri zote kuhakikisha Hoja zote za CAG zinapatiwa majibu, kuhakikiwa na kufungwa, ushirikiano unatolewa kwa CAG na taratibu za kufunga hoja zinazingatiwa.

Halkadhalika  Mhe. Kandege alimpongeza aliyekuwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali Ndugu Mohamed A. Mtonga kwa kustaafu utumishi wa umma na kazi kubwa aliyoifanya katika kada hii ya ukaguzi.

“Ndugu Mohamed nakutakia Afya njema, naamini bado una nguvu za kuendelea kutoa mchango wako kwenye shughuli za kiuchumi za kujenga Taifa letu endelea kuwa Mwalimu kiongozi kwa wakaguzi wa ndani, ukiendelea kuwafundisha na kutoa ushauri, nakutakia kila la Kheri.  Alisema Kandege.

Akizungumza wakati wa Mkutano huo Karibu Mkuu OR-TAMISEMI Eng. Joseph Nyamhanga amesema  kutokana na umuhimu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani fedha zilizotengwa kwenye bajeti kwa ajili ya Kitengo hiki zitalindwa na kuhakikisha zinatumika kwa ajili ya kazi za kitengo hiki pekee.

“Umefika muda sasa vitengo vya wakaguzi wa ndani kuimarishwa na Kila Mkoa na Halmashauri kuviwezesha vitengo hivi rasilimali fedha, watu na vitendea kazi vya kutosha wakati wote” Alisema Nyamhanga.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ukaguzi na Ufuatiliaji Ofisi ya Rais TAMISEMI Miriam Mbanga amesema Mkutano wa kazi kwa wakaguzi wa ndani wa Mikoa na Halmashauri wa kwanza kufanyika na unalenga kujifunza, kubadilishana uzoefu, kushirikishana namna mbalimbali ya kutatua changamoto za kiukaguzi na kujiwekea malengo ya namna ya kufanya kazi ya ukaguzi wa ufanisi.

Mkutano huu umehudhuriwa na Wakaguzi wa Ndani zaidi ya mia moja na hamsini kutoka katika Sekretariet za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post