RAIS MAGUFULI AMUAHIDI RAIS WA DRC KUTOWAONDOA WANAJESHI WA TANZANIA

Rais  Magufuli amesema kitendo cha wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kumpa dhamana Felix Tshisekedi kuiongoza nchi hiyo kimeweka historia mpya ya kufanya uchaguzi wa amani na demokrasia huku akibainisha kuwa demokrasia inaendelea kuota mizizi Afrika.

Hayo ameyasema jana Alhamisi ya Juni 13, 2019 katika hafla aliyoiandaa kwa ajili ya rais huyo ambaye atakuwa nchini kwa ziara ya siku mbili.

Magufuli alisema tangu nchi hiyo kupata uhuru wake ni mara ya kwanza uchaguzi umefanyika kwa haki, amani na kwa demokrasia ya hali ya juu.

“Nikupongeze wewe pamoja na aliyekutangulia, hakika mmefanya jambo kubwa la kukumbukwa na kuwekwa katika vitabu vya kihistoria, hongereni sana,” alisema Magufuli.

Akizungumzia ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo mbili amesema licha ya kuwa hadi sasa wanajeshi 30 wa Tanzania wamepoteza maisha wakati wakilinda amani DRC, lakini bado Tanzania itaendelea kupeleka wanajeshi kuhakikisha nchi hiyo inakuwa salama.

“Kwa jinsi unavyojitahidi kutengeneza amani kwa kuunganisha vikundi mbalimbali ikiwemo kuwafungulia wafungwa wa kisiasa ni hatua nzuri na sisi tutaendelea kukuombea ili amani itengemae kwa sababu siyo kwa ajili yenu tu bali hata nchi za maziwa makuu tutanufaika,” alisema Magufuli.

Alisema anaamini ziara ya rais huyo itazaa matunda na akamtaka kujisikia na amani akiwa nchini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527