MWANAMKE ALIYEPATIWA USINGIZI MZITO AJIKUTA PEKE YAKE NDANI YA NDEGE…..NDOTO ZA AJABU ZATAWALA

Mwanamke mmoja amesema aliachwa peke yake ndani ya ndege baada kuangusha usingizi mzito akiwa safarini.

Tukio hilo limemkuta Bi Tiffani Adams Juni 9 mwaka huu ambaye alikuwa akisafiri kwa kutumia Shirika la Ndege la Canada kutoka jiji la Quebec kwenda jiji la Toronto.

Alipoamka, alijikuta yumo ndani ya baridi kali, huku bado akiwa amefunga mkanda wa kiti chake, lakini ndege ilikuwa imeegeshwa na ta zote zimezimwa.

Amesema amekuwa akipatwa na "ndoto za kutisha" toka tukio hilo lilipomtokea.

Shirika la Ndege la Canada limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanafanya uchunguzi.

Bi Adams ameandika kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook aliamka "mishale ya saa sita usiku (saa chache baada ya ndege hiyo kutua) nilikuwa kwenye baridi kali huku nikiwa bado nimechomeka mkanda wangu kitini, na kiza totoro."

Amesema hali hiyo ilikuwa ya "kuogopesha".

Bi Adams alifanikiwa kumpigia simu rafiki yake, Bi Deanna Dale na kumfahamisha mahala alipo na kabla hawajamaliza kuongea, simu yake ilizimika kwa kuishiwa chaji.

Hakuweza kuchaji simu yake kwani ndege ilikuwa imezimwa.

Bi Dale alifanikiwa kuwapigia simu polisi wa Uwanja wa Ndege wa Toronto Pearson na kuwaarifu juu ya masaibu ya rafiki yake na mahala alipo.

Akiwa amekwama ndani ya ndege, Bi Adams aliweza kuona kurunzi kwenye eneo la rubani na akajaribu kuiwasha ili watu waone kuna kitu ndani ya ndege hiyo.

Alionwa na dereva wa vigari vya kupakua mizigo ya wasafiri, ambaye anasema alipigwa na butwaa kumuona.

Bi Adams anasema wafanyakazi wa Shirika la Ndege la Canada walimpatia gari la kifahari na chumba cha hoteli baada ya kumnasua kutoka kwenye ndege hiyo lakini akawagomea, akitaka kurejea nyumbani kwa haraka iwezekanavyo.

Amesema mwakilishi wa shirika hilo amempigia mara mbili ikiwa kama sehemu ya uchunguzi na kumuomba radhi.

Shirika hilo limekiri kutokea kwa tukio hilo kwenye vyombo mbalimbali vya habari na kudai wanaendelea na unchunguzi wa kisa hicho.
Chanzo- BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post