MOHAMMAD MORSI AZIKWA KIMYA KIMYA CAIRO, MISRI

Rais wa zamani wa Misri Mohammed Morsi amezikwa leo, baada ya hapo jana kuanguka mahakamani na kuaga dunia. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yametaka kufanyika uchunguzi huru, kufahamu sababu halisi ya kifo chake.

Wakili wa rais huyo wa zamani amesema Morsi amezikwa leo asubuhi katika makaburi ya Medinat Nasr Mashariki mwa mji mkuu, familia yake ikiwepo. Televisheni ya taifa imesema kifo chake kilisababishwa na mshituko wa moyo.

Morsi, rais wa kwanza wa kiraia wa Misri, ambaye ni wa kwanza pia kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, alianguka katika kizimba chake mahakamani baada ya kujieleza, na aliwahishwa hospitalini ambako ilitangazwa kuwa alikuwa tayari amekata roho.

Tangu alipoangushwa katika mapinduzi ya kijeshi Julai 2013, aliyekuwa waziri wake wa ulinzi Abdel Fattah al-Sisi amechukua hatamu, na amefanya ukandamizaji mkubwa dhidi ya maelfu ya wanachama na wafuasi wa kundi la Udugu wa Kiislamu, mamia miongoni mwao wakikabiliwa na hukumu ya kifo.

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Misri wamesema yumkini mazingira mabaya gerezani yamesababisha kifo cha Morsi, hali ambayo wanasema ni ukiukaji wa haki za binadamu. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post