GENGE LA MAJAMBAZI LAACHIA VIDEO LIKIWATISHIA POLISI


Kanda ya video ya kiongozi wa genge moja la majambazi kwa jina Gaza akijigamba kuhusu uhalifu aliotekeleza imesambaa katika mitandao ya kijamii na kuwawacha wengi vinywa wazi

Kulingana na gazeti la The Standard nchini Kenya kiongozi huyu wa genge ambaye polisi wanamtambua kwa jina Seba Alias Johnnie alionekana katika kanda hiyo ya video akijigamba kwamba bado yeye ndiye mfalme wa uhalifu nchini Kenya na kwamba hakuna kile ambacho polisi wataweza kufanya.

Katika video hiyo Seba ambaye alikuwa akitekeleza operesheni zake kutoka eneo la Mlango Kubwa jijini Nairobi anasikika akiwatishia maafisa wa polisi kwamba atawashambulia na visu.

Kiongozi huyo wa gengi ambaye kwa sasa anadaiwa kutekeleza uhalifu wake kutoka kaunti ya Tana River anaendelea kujigamba kwamba kufikia sasa ameweza kuiba simu 86 kutoka kwa raia na kwamba maafisa wa polisi walifanya makosa kwa kudai kwamba ameiba simu 46 pekee.

Kulingana na gazeti hilo Jamaa huyo anayejiita Mfalme wa Gaza anaendelea kuelezea kwamba hatosita kutekeleza uhalifu hivi karibuni na kwamba polisi wanaweza kumtafuta.

Seba ambaye alikuwa ameandamana na wenzake wanne katika video hiyo amewaonya raia wanaopeleka ujumbe kwa polisi kwamba atawashambulia kwa visu iwapo wataendelea kufanya hivyo.
Mitandao ya kijamii

Wakenya katika mitandao ya kijamii wamewataka polisi kumtafuta Seba na kundi lake wakidai kwamba wameyafanya maisha ya wakaazi wa Nairobi kuwa magumu.

''Maafisa wa polisi wanatakiwa kuchukua hatua za haraka kabla ya kutekeleza vitisho vyao'', Robert Jakoriw aliandika katika mtandao wa facebook.

''Je DCI kinoti yuko wapi, hawa vijana wanafaa kuchukuliwa hatu'' , alisema Frank Rapemo mtumiaji mwengi wa mtandao wa Facebook.
Uhalifu

Eneo la Kayole jijini Nairobi limesemekana kuwa nyumbani kwa wanachama wa Genge hilo la Gaza , ambalo ni mojawapo ya megenge yanayoogopwa sana eneo la Eastaland.

Wakaazi wengi katika eneo hili wanaishi chini ya dola moja kwa siku , hatua inayowashinikiza vijana wengi kujiingiza katika uhalifu.

Kulingana na gazeti la The Standard nchini Kenya genge hilo la Gaza linaaminika kutekeleza idadi kadhaa ya mauaji na uhalifu katika eneo hilo lakini operesheni zake hazijulikani.

Wanachama wake hutumia visu na bunduki kama vifaa vya biashara yao.

Genge hilo pia linadaiwa kuanzisha genge jingine la Yakuza ambalo uhusika na uhalifu wa hali ya juu kama vile wizi wa benki na ule wa barabara kuu.

Mapema mwaka huu, maafisa wa polisi walikiri kwamba kundi hilo limekuwa likiwatishia wakaazi lakini wamesema kuwa wanatumia kila njia kuimarisha usalama wa wakaazi wa eneo hilo.
Chanzo - BBC
SOMA ZAIDI HAPA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post