LUGOLA: MWANAMKE ANAYEFIKISHWA POLISI HAPASWI KUKAGULIWA NA ASKARI WA KIUME


Serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani Nchi, Kangi Lugola imesema mtuhumiwa mwanamke anayefikishwa kituo cha polisi hapaswi kukaguliwa na askari wa kiume, kwamba kazi hiyo inapaswa kufanywa na askari wa kike, mgambo wa kike au mke wa askari aliyepo karibu na eneo husika.

Lugola ametoa kauli hiyo  leo Jumatatu Juni 24, 2019 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Geita (CCM), Joseph Kasheku ‘Musukuma’ aliyetaka kujua ni lini askari wa kike watapelekwa katika kituo cha polisi Nkome kwa maelezo kuwa kituoni hapo upekuzi kwa akina mama hufanywa na askari wa kiume.

“Nimeshamuagiza RPC (Kamanda wa polisi Geita) kupeleka askari wa kike katika kituo hicho. Taratibu zinaruhusu upekuzi kwa wanawake kufanywa na askari wa kike na kama hayupo basi kazi hiyo ifanywe na mgambo wa kike au mke wa askari,” amesema Lugola.

Katika swali la msingi, Musukuma alihoji sababu za kituo hicho kutokuwa na askari wa kike na kujibiwa na naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masuani kuwa vituo vya polisi Nkome, Nyamboge, Kakubilo na Nzela havina askari wa kike kutokana na ukosefu wa miundombinu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post