KIPIGO CHA TAIFA STARS CHAIBUKIA BUNGENI DODOMA

RAMADHAN HASSAN-MTANZANIA DODOMA
Kipigo cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ dhidi ya Senegal kimeibukia bungeni ambapo mbunge wa Mbozi, Paschal Haonga, (Chadema) ameomba muongozo bungeni akihoji ni kwanini wachezaji wa Stars wamekatwa posho na Serikali akidai kuna tetesi kwamba wachezaji wa Taifa Stars walitakiwa kupewa posho ya Dola 300 za Marekani kwa siku lakini Serikali imewapa Dola 70.

Mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu bungeni leo Juni 24, Haonga alisimama na kuomba muongozo kwa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson akitaka apewe majibu ni kwanini wachezaji wa Stars wamekatwa posho zao

“Mheshimiwa Naibu Spika jana kulikuwa na mechi kati ya timu yetu ya Taifa na Senegal na tulifungwa mabao 2-0 hali hii kwa watanzania wengi hasa wapenda soka wamelala na maumivu makubwa. Kuna tetesi ambazo zinaendelea katika mitandao ya kijamii kwamba Serikali ingeweza kuipatia Taifa Stars dola 300 kwa siku kule Misri lakini taarifa zilizopo ni kwamba wamepewa dola 70 hivyo inaonekana hawajalipwa hela zao kama wanavyotakiwa kulipwa kila siku,” amesema.

Haonga amedai kwamba kuna mgomo wa kimya kimya katika timu hiyo na kuna siku wachezaji waligoma kufanya mazoezi.

“Ninaamini unapoingia katika michezo lazima uwe na morali ili uweze kucheza vizuri na hali hii ilipelekea siku moja wachezaji kugoma kufanya mazoezi kwahiyo mgomo wa kimya kimya kama unaendelea vile.

Akijibu swali hilo Dk. Tulia amesema hawezi kujibu jambo hilo kwa sababu halijatokea ndani ya Bunge.

“Waheshimiwa Wabunge kanuni ya 68 fasihi ya saba inataka kiti kitoe muongozo kwa jambo ambalo limetokea bungeni mapema, jambo hili halijatokea hapa bungeni,” amesema

Jana Stars ilikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Senegal katika Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Misri.
Chanzo - Mtanzania

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527