DK. KIGWANGALLA KUCHANGISHA FEDHA ZA KUTOKOMEZA VVU KUPITIA MLIMA KILIMANJARO


Waziri wa Maliasili na Utalii. Dk. Hamis Kigwangalla (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), Richard Jordinson katika hafla ya uzinduzi wa zoezi la kupanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kukusanya fedha za kutomomeza maambukizi ya VVU nchini. Zaidi wa wapandaji 80 wameshiriki kampeni hiyo inayoratibiwa na GGM kwa kushirikiana na Tacaids.
Waziri wa Maliasili na Utalii. Dk. Hamis Kigwangalla (wa pili kushoto) akiwa pamoja na baadhi ya viongozi na washiriki wa kampeni ya kupanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kukusanya fedha za kutomomeza VVU nchini. Kampeni hiyo iliyodumu kwa miaka 17 sasa imeratibiwa na Mgodi wa dhahabu GGM na Tacaids.
Baadhi ya washiriki wa kampeni ya kupanda Mlima Kilimanjaro 'Kili challenge 2019' inayoratibiwa na GGM kwa kushirikiana na TACAIDS kwa lengo la kukusanya fedha za kutokomeza maambukizi ya VVU na Ukimwi nchini. Zoezi la upandaji mlima huo limezinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla.
***

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Khamis Kigwangala amesema anatarajia kuandaa utaratibu wa makundi ya watu mbalimbali wakiwamo viongozi mashuhuri na wasanii kupanda mlima Kilimanjaro ili kuchngisha fedha za kuendeleza mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi.

Dk. Kigwangala ametoa kauli hivi karibuni mkoani Kilimanjaro wakati akizindua zoezi la upandaji Mlima Kilimanjaro lililoshirikisha zaidi ya watu 80 kutoka nchi mbalimbali kwa lengo la kuchangisha fedha za mapambano dhidi ya Ukimwi kwa kupitia kampeni ya ‘Geita Gold Mining Kilimanjaro Challenge 2019’.

Kampeni hiyo ambayo iliyoratibiwa na Mgodi wa dhahabu ya Geita (GGM) kwa kushirikiana na Tume ya kudhibiti Ukimwi nchi (TACAIDS) pia imelenga kutunisha mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF).

Alisema wizara ya maliasili na utalii itaanda utaratibu wa kuhamasisha makundi ya watu mbalimbali ikiwemo wasanii na watu mashuhuri duniani kupanda Mlima Kilimanjaro ili kuchangisha fedha za mapambano dhidi ya Ukimwi kwani mapambano ya virusi hivyo ni ya watu wote na sio ya serikali pekee.

“Takwimu za maambukizi mapya hususan katika kundi la vijana yanatisha na kwamba zinahitajika jitihada za makusudi kutoka Katika kundi hilo kudhibiti ugonjwa huo.

“Hali ya maambukizi mapya ya VVU yanatisha ni lazima sisi Kama vijana tuwe msitari wa mbele kupambana na hali hii, kwa mwaka nimepanga kupanda Mlima huu na watu mashuhuri ikiwemo wanasiasa na wasanii ili kuchangisha fedha kwa ajili ya kudhibiti ugonjwa huu.

“Lakini pia nimefurahi kuona kuwa miongoni mwa wanufaika wa kampeni hii ni wapagazi takribani 150 waliopatiwa mafunzo ya kujilinda na VVU na masuala mbalimbali kuhusu udhibiti wa Ukimwi. Kundi hilo pia limepatiwa mafunzo ya ujasiriamali kwa lengo la kuwasaidia wawe na kipato endelevu,” alisema. 

Aidha, Mkurugenzi wa Tacaids, Dk. Leonard Maboko, alisema kila siku watu zaidi ya 200 huambukizwa VVU ambapo Kati yao asilimia 80 ni vijana kuanzia miaka 15-24.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) Richard Jordinson, kampeni hiyo imewezesha ukusanyaji wa zaidi ya Sh bilioni 13 tangu ilipoanzishwa miaka 17 iliyopita.

Alisema kampeni ya mwaka huu zaidi ya watu 80 wameshiriki ambapo kati yao 32 watapanda mlima, 28 watauzunguka kwa kutumia baiskeli na watu 17 kutoka nchi mbalimbali wameshiriki kampeni hiyo ya kupanda mlima Kilimanjaro.

“Upandaji huo utachukua siku saba ambapo wameanza kupanda Juni 15 na kushuka Juni 22 mwaka huu,” alisema

Alisema tangu kuanzishwa kwa kampeni hiyo miaka 17 iliyopita zaidi ya taasisi binafsi na mashirika 50 yanayotoa misaada na elimu ya Ukimwi nchini yamenufaika na kampeni hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527