JESHI LA POLISI KIGOMA LAFANIKIWA KUMKAMATA KINARA WA UBAKAJI NA KUJERUHI WANAWAKE

Vyombo vya dola mkoani Kigoma vimefanikiwa kumkamata Hussein Hamis, anayetuhumiwa kuwa kinara wa ubakaji na kujeruhi wanawake nyakati za usiku maarufu kama teleza.


Hamis aliye maarufu kwa jina la Orosho, alikamatwa pamoja na watuhumiwa wengine tisa wakitambuliwa kama teleza, ambao huwaingilia kingono wanawake kwa kuwalazimisha, kuwaibia na kuwajeruhi wakiwa wamejipaka ‘oil’ chafu au mafuta ya mawese ili wanaposhikwa wawe wanateleza.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mjini, Samson Hanga alisema baada ya kuwapo taarifa hiyo, vyombo vya dola viliendesha  msako mkali kwa kushirikiana na wananchi ili kuwakamata wahalifu.

“Tulitengeneza namna bora ya kuwakamata wahusika, tulifanya kazi ya upigaji kura ya siri tukapata majina, mengine tulipata kupitia vyombo vya dola. Mpaka sasa tumekamata vijana tisa, wapo mahabusu na upelelezi unaendelea,” alisema Hanga.

Alisema katika majina yaliyotajwa na kupigiwa kura, mtuhumiwa mmoja alitajwa na akina mama waliofanyiwa vitendo vya ukatili ambaye ni Hamis.

“Unajua Serikali ina mkono mrefu, macho makubwa, yule kijana alipopata taarifa tunamtafuta alikimbilia kwa mama yake Kijiji cha Kagongo, baadae akakimbilia tena Kijiji cha Kagunga, juzi jioni tukafanikiwa kumkamata wilayani Kasulu na kuletwa hapa kituo cha polisi kwa ajili ya hatua zaidi,” alisema.

Hanga alisema pia wamefanya gwaride la utambuzi kwa waathirika  kuwatambua vijana 10 waliokamatwa.

Alisema msako bado unaendelea na kuonya yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja kabla vyombo vya dola havijambaini na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale wote watakaobainika.
.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post