SERIKALI YA KENYA YAMPOTEZEA MBUNGE WA STAREHE 'JAGUAR' ALIYETISHIA KUFUKUZA WATANZANIA

 Serikali ya Kenya imewahakikishia wafanyabiashara wa kigeni nchini humo usalama wakati wote huku ikisema Serikali haipo upande wa Mbunge wa Starehe, Charles Njagua maarufu Jaguar kuhusu kauli alizozitoa.

Mbunge huyo ambaye pia ni mwanamuziki kupitia mitandao ya kijamii jana Jumanne ilisambaa video yake akieleza kuwafukuza wafanyabiashara wa kigeni wakiwemo Watanzania ndani ya masaa 24 kurudi kwao la sivyo watawapiga na kuwarudisha nchini mwao.

Taarifa iliyotolewa jana Jumanne Juni 25, 2019 na Msemaji wa Serikali ya Kenya, Cyrus Oguna imelaani kauli ya Jaguar na kueleza haikubaliki katika kipindi hiki cha utandawazi.

“Wakenya ni watu wenye upendo na amani ambao kwa miaka mingi wameshirikiana na mataifa mbalimbali. Hii ni tunu tunajivunia na tutaendelea kushirikiana,” imeeleza taarifa.

Oguna amesisitiza usalama wa mali na watu kutoka mataifa mbalimbali pindi watakapo wekeza katika nchi hiyo utaendelea kama ulivyo sasa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa akitoa kauli ya Serikali bungeni kuhusu kauli hiyo ya Jaguar, kiongozi huyo aliwatoa hofu Watanzania baada ya kusema wamewasiliana na Ubalozi wa Kenya nchini Tanzania ambao ulisisitiza Serikali kutohusika na maneno ya Jaguar.
Na Muyonga Jumanne, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post