BARABARA ZAWATIA HOFU MADIWANI NZEGA KUTOCHAGULIWA KATIKA UCHAGUZI WA 2020


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nzega Seleman Sekeite akielezea maendeleo ya halmashauri yake.
Kipande cha barabara wilayani Nzega kinacholalamikiwa na madiwani
Wajumbe wa baraza la madiwani wakiendelea na kikao cha kujadili maendeleo ya miundombinu ya halmashauri ya wilaya ya Nzega.
Jengo La Halmashauri ya Wilaya ya Nzega ambapo Mkutano wa Baraza la Madiwani umefanyikia.

Na Joshua Kasase Tabora

Tatizo la barabara katika halmashauri ya wilaya ya Nzega mkoani Tabora bado linaendelea kugonga vichwa vya viongozi wengi wilayani humo huku baadhi ya madiwani wakihofia kutokuchaguliwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ikiwa ahadi zao kubwa kwa wapiga kura wao ni uboreshaji wa barabara hizo ambazo bado miundo mbinu yake ni mibovu.

Wakizungumza katika kikao cha baraza la madiwani eo katika ofisi za halmashauri ya wilaya ya Nzega wamesema changamoto ya barabara inawafanya waonekane waongo kwa wapiga kura wao hivyo kuhofia kutochaguliwa kwenye uchaguzi ujao.

Baadhi ya madiwani akiwemo Kitambi Luziga, Mihayo John wamesema barabara ndiyo hoja kuu kwao.

"Ni bora mimi nikose kila kitu kwenye bajeti ya mwaka unaokuja mnisitishieni mambo mengine yote ila mnipe barabara katika kata yangu, bora angalau kuliko miaka mitano hakuna hata kitu" amesema Luziga.

"Hii Barabara inanipa mtihani mzito sana maana ukizingatia wananchi wangu walishafyeka hadi visiki ila bado hakuna chochote ambacho kimeshafanyika hadi sasa",ameongeza John.


Nao  Lufunga Kasheshi na Mdoda Jumanne wamelezea hofu yao kubwa kuwa ni baadhi ya maeneo kama mto Mvigombo kijiji cha Nongo na barabara zinazotumiwa na wafanya biashara wengi katika maeneo yao hazitajegwa na kudai huenda kutokamilika kwa ahadi zao huenda wakapigwa chini na wapiga kura wao.

Meneja wa TARULA wilaya ya Nzega, Nestory Tibanya amesema mtandao wa barabara ni kilometa 1,247.6.8  na kwamba ufinyu wa bajeti ndiyo tatizo.

"Ufinyu wa Bajeti ndio tatizo hivyo kulingana na ufinyu huo pamoja na ukomo wa bajeti ndiyo maana unakuta tunaangalia zile barabara za muhimu sana ndizo tunazishughulikia, ndio maana inaonekana zimetengenezwa barabara chache",amesema Tibanya.

Hata hivyo, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nzega Selemani Sekeite  amesema licha ya changamoto zote hizo bado kasi ya maendeleo katika wilaya hiyo zinaendelea kusonga mbele, hasa katika idara ya elimu,afya na hata ukusanyaji wa mapato unaridhisha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post