Simba imeitwanga Coastal Union kwa mabao 8-1 katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyomalizika hivi punde kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Pamoja na ushindi wake mnono, washambuliaji wake wawili, Emmanuel Okwi na Meddy Kagere kila mmoja amefunga mabao matatu, yaani hat trick.
Kwa mabao hayo, Kagere amefikisha mabao 20 msimu katika ligi kuu huku Okwi akifikisha 14 na kulingana na nahodha wa Simba, John Bocco aliyekuwa benchi katika mechi ya leo.
Mabao mengine yalifungwa na Hassan Dilunga na Cleotus Chama raia wa Zambia na kuifanya Simba iandike ushindi huo mnono zaidi.
Kwa ushindi wa leo, Simba imefikisha pointi 81 na kupaa kileleni ikiwaacha Yanga wenye pointi 80 waliokuwa wamekaa kileleni kwa muda mrefu zaidi.
Yanga wamecheza 34 huku Simba wakiwa wamefikisha mechi 31 baada ya kucheza mechi yao ambayo wametoa kipigo kikali kwa Wagosi wa Kaya.