SERIKALI INAFANYA MAZUNGUMZO NA CYPRUS ILI KUWALIPA WATEJA WA BENKI YA FBME

Na. Peter Haule na Josephine Majura, WFM, Dodoma

Serikali ya Tanzania inafanya mazungumzo na Serikali ya Cyprus ili kuweza kutatua changamoto za malipo kwa wateja walioweka amana zao katika Benki ya FBME ambayo ilifutiwa leseni ya kufanya shughuli za kibenki hapa nchini na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Viti maalaum  Mhe. Asha Abdullah Juma, alieuliza kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali kuwasaidia wananchi walioweka amana zao katika Benki ya FBME.

Dkt. Kijaji alisema kuwa zoezi la kukusanya mali na fedha zilizokuwa za Benki ya FBME katika taasisi mbalimbali za fedha hasa zilizopo nje ya nchi, limekumbwa na changamoto za kisheria kati ya Tanzania na Cyprus ambako benki ya FBME ilikuwa ikiendesha sehemu kubwa ya biashara zake hivyo kusababisha ucheleweshaji wa ukusanyaji na ugawaji wa fedha na ufilisi.

“Hakuna tarehe rasmi ya kuanza kulipa fedha kwa sasa kutokana na uwepo wa kesi zinazokwamisha zoezi la ukusanyaji mali na madeni ya Benki ya FBME”, alieleza Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa, Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 inaeleza kuwa amana au akiba za wateja katika Benki au Taasisi zina kinga ya Bima ya Amana ya kiasi kisichozidi Sh. milioni 1.5,  na iwapo mteja ana salio la amana la kiasi kisichozidi Sh. 1.5 atapata fidia ya asilimia 100.

Aidha wateja walio na zaidi ya Sh. milioni 1.5 wanalipwa Sh. milioni 1.5 kama fidia ya bima ya amana na kiasi kinachobakia kinalipwa kwa mujibu wa Sheria na taratibu za Ufilisi.

Hata hivyo malipo kwa mujibu wa Sheria na taratibu za ufilisi yanategemea makusanyo ya fedha kutoka kwenye mauzo ya mali pamoja na fedha zilizowekwa na benki katika taasisi mbalimbali za fedha za ndani na nje ya nchi.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527