SERIKALI YAFANIKIWA KUPELEKA HUDUMA ZA KIBENKI VIJIJINI

Na. Peter Haule na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma

Serikali imesema kuwa Vituo vyote vya huduma ndani ya Ofisi za Shirika la Posta vimeunganishwa kwenye mtandao na mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano- TEHAMA wa Benki ya TPB  kwa wateja wa vijijini na pembezoni mwa miji, ili kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa wakati kama ilivyo kwa wateja wengine wanaohudumiwa na matawi makubwa na madogo.

Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa wa Tumbatu Mhe. Juma Othman Hija, aliyetaka kujua iwapo Benki ya TPB imefikia malengo ya kupeleka huduma vijijini na maeneo yasiyofikika kwa urahisi.

Dkt. Kijaji alisema kuwa lengo la Benki ya TPB ni kuongeza wigo  wa biashara ya benki kwa kutumia teknolojia ya kisasa katika maeneo ya vijijini, hivyo Benki hiyo imefanikiwa kuboresha huduma katika ofisi 200 za Shirika la Posta Tanzania kwa kutumia teknolojia ya TEHAMA inayomuwezesha mwananchi kupata huduma za kibenki kupitia simu za kiganjani, mawakala wa kampuni za simu pamoja na mashine za kutolea fedha (ATM) .

“Benki ya TPB  imeongeza idadi ya matawi makubwa kutoka 30 kwa mwaka 2017 hadi 36 kwa mwaka 2018 na matawi madogo yaliongezeka  kutoka 37 mwaka 2017 hadi kufikia 40 kwa mwaka 2018, yakiwa yanawawezesha wateja kupata huduma bila kutembelea matawi walipofungulia akaunti zao”, alieleza Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa Idadi hiyo ya matawi inahusisha matawi yaliyokuwa ya Benki ya Twiga na Benki ya Wanawake Tanzania, aidha jumla ya akaunti 227,052 zilifunguliwa na wananchi wa vijijini na pembezoni mwa miji kwa kutumia mfumo wa kibenki kwa njia ya simu za kiganjani unaojulikana kama TPB Popote.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527