MKURUGENZI WA UCHAGUZI DKT. KIHAMIA ARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA WATUMISHI WA NEC

Hussein Makame

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Dkt. Athumani Kihamia ameeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa watumishi wa tume hiyo kutokana na kufanya kazi kwa bidii, ushirikiano, weledi na uzalendo.

Dkt. Kihamia ameeleza hayo wakati alipokutana na wafanyakazi wa NEC kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kujadili mambo mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya Tume.

Alisema katika kipindi alichokaa Tume amegundua kuwa sasa utendaji kazi wa mazeoa umepungua na watumishi wengi wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa wakati, kwa uaminifu, kutunza siri na kuepuka matumizi ya fedha yasiyo ya lazima.

Mkurugenzi huyo wa NEC alifafanua kuwa katika kikao chake cha kwanza na watumishi wa Tume cha Agosti 7 mwaka 2018, alijadili changamoto zinazowakabili watumishi hao ambazo zilikuwa kikwazo cha utekelezaji wa majukumu yao kwa njia moja au nyingine.

“Tuligundua kuwa changamoto nyingi zilitokana na tabia binafsi za baadhi ya watumishi, na baadhi yao kufanya kazi kwa kuigiza yaani kwa mazoea kwa kisingizio cha mchakato”, alisema Dkt. Kihamia na kufafanua kuwa:

“Lakini sasa hivi jambo la kufurahisha asilimia kubwa ya watumishi wanafanya kazi sio kwa mazoea, lakini pia ufanisi wa kazi zao umeongezeka kwa kiwango kikubwa”.

Alibainisha kuwa kwa sasa Tume imeimarika vya kutosha kwa kuwa wakati alipofika wastani wa utendaji kazi ulikuwa asilimia 52, ikimaanisha kuwa zaidi ya asilimia 48 ya watumishi walikuwa hawawajibiki ipasavyo, lakini sasa uwajibikaji umefikia wastani wa asilimia 65 baada ya kuwekeana malengo.

“Kwa hiyo tulipo sasa tupo juu ila ni lazima tuendelee kuwa kitu kimoja, ingawa katika kuimarika huko wapo wenzetu wachache sana wenye matatizo madogo madogo, hivyo wanatakiwa warekebishwe” alisisitiza Dkt. Kihamia

Alifafanua kuwa kuimarika kwa utendaji kazi ni jambo kubwa kwa maendeleo ya nchi kwa kuwa kutowajibika ipasavyo kwa watumishi wa umma katika nchi nyingi za Afrika kumesababisha udumavu wa maendeleo ya nchi hizo.

Hivyo aliwataka watumishi wa NEC kuendeleza tabia ya uwajibikaji kwa mustakbali wa maendeleo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tanzania kwa ujumla kwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuwa chachu ya maendeleo ya nchi.

Ili kuboresha zaidi utendaji kazi wa Tume, Dkt. Kihamia aliziagiza kila idara ziainishe vipaumbele (priorities) vitakavyotekelezwa na idara husika kwa kipindi chote kuanzia Julai 1 mwaka huu.

Alisema baada ya kupata vipaumbele hivyo kutoka kila idara vitaunganishwa kupata vipaumbele vya Tume na aliwataka watumishi kutambua kuwa majukumu ya kila idara ni majukumu ya Tume hivyo ni muhimu kuwa kitu kimoja katika kuyatekeleza.

“‘Checklist’ ni jambo kubwa sana kwa sababu kuna mtu ukienda kwenye idara yake ukimuuliza amefanya mambo gani, anaweza akawa amefanya mambo mazuri tu lakini hayakumbuki mpaka ayafikirie ndio akwambie” alisema Dkt. Kihamia na kufafanua kuwa:

Alisema checklist ni mpango kazi ambao hata watafiti wanaofanya tafiti za kisasa wamegundua kwamba kampuni nyingi za kibiashara zinazofilisika ni zile ambazo hazina checklist za kisasa.

“Kwa hiyo checklist ni moja ya agenda ambayo nimekuja kuizungumzia leo kwa sababu tunafanya kazi kwa mipangokazi na unapokuwa na checklist unajua hili nimelifanya hili sijafanya” alisema Dkt. Kihamia.

Alisema mtumishi asipokuwa na checklist ya kazi zake hawezi kuwa na muendelezo (consistency) mzuri wa majukumu ambayo mtumishi anataka kuyatekeleza na ukamilifu wa kazi zake hautakuwepo.

Alisema wataalamu wanasema kwamba checklist ndio njia pekee kwa sasa inayoaminika katika kutekeleza majukumu kwa ufasaha.

“Mtafiti mmoja aliwahi kusema checklist ni aina ya mpangilio wa majukumu ambao unapunguza kushindwa (failure)katika kazi, ina maana usipokuwa na checklist uwezekano wa kushindwa ni mkubwa” aliongeza Dkt. Kihamia.

Kwa upande mwingine Dkt. Kihamia alimtaka kila mtumishi wa Tume atambue majukumu ya msingi ya NEC na ikiwemo kufahamu Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni nini na kufahamu taratibu zote za uchaguzi.

“Watu wajifunze kuwepo kwa nafasi wazi ni nini maana watu wanalalamika kwamba Serikali inatumia fedha nyingi kufanya chaguzi ndogo za mara kwa mara lakini wanasahau kwamba suala hilo lipo kwenye katiba na ni utarabu.” alisema Dkt. Kihamia.

Dkt. Kihamia tangu alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi amejiwekea utaratibu wa kukutana na watumishi wa tume hiyo huku hiki kikiwa ni kikao chake cha tatu.

Katika kikao cha kwanza cha tarehe 7 Agosti mwaka 2018, Dkt. Kihamia aliainisha vipaumbele vyake 30 vya kuzingatia katika utekelezaji wa majukumu ya Tume na kuvifanyia tathmini kwenye kikao cha pili kilichofanyika mwezi Desemba mwaka 2018.

Baadhi ya vipaumbele alivyosisitiza ni kuweka mpango kazi wa kila idara, kitengo na mtumishi na utekelezaji wake kwa kile mwezi, kuandaa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya kila idara, kutambua madeni ya kila idara na kitengo na kuonesha kama yamehakikiwa au la, sababu ya madeni hayo na kuwepo rejesta na mpango kazi wa malipo.

Katika vikao hivyo wakuu wa Idara wamepewana nafasi ya kufafanua mambo mbalimbali katika idara zao na watumishi kuwepo nafasi ya kueleza mambo mbalimbali kuhusu utekelezaji wa majukumu yao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post