KANYASU AAHIDI MIRADI YA MAENDELEO ITAKAYOTEKELEZWA MJINI GEITA ITAFUATA TARATIBU ZOTE

NA LUSUNGU HELELA

Mbunge wa Geita Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu,ametoa ahadi ya kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo itakayotekelezwa mwakani katika Halmashauri ya Mji wa Geita  itazingatia taratibu zote zinazotakiwa ili isiweze kukataliwa.

Kauli hiyo imekuja mara baada ya mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu kubaini baadhi ya kasoro katika miradi iliyotekelezwa katika Halmashauri hiyo hali iliyolazimu  mradi wa maji  kushindwa kuzinduliwa.

Hayo ameyasema wakati alipokuwa akizungumza na Wananchi wa Kasamwa katika eneo ambalo mkesha wa Mwenge ulipofanyikia  katika Halmashauri ya Mji wa Geita mkoani Geita.

Kufuatia hali hiyo ya  mradi wa maji kushindwa kuzinduliwa unaodaiwa  kugharimu shilingi bilioni sita,  hali hiyo  imempelekea Kiongozi wa mbio za Mwenge wa mwaka huu, Mzee Mkongea Ally kuiagiza  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  kuchunguza mradi huo .

Mhe.Kanyasu amesema mwaka huu ukimbizaji Mwenge umekuwa na maana kubwa  kufuatia kufanya ukaguzi usiotia shaka kwenye miradi iliyotekelezwa na pale wanapobaini ukiukwaji miradi hiyo imekuwa haizinduliwi.

" Ukaguzi mnaoufanya katika miradi hii ni ishara tosha kabisa kuwa mmekuja kufanya kazi kwa ajili ya wananchi'' alisisiiza Kanyasu

Amesema miaka ya nyuma zoezi la ukimbizaji Mwenge lilikuwa la kawaida hali iliyopelekea kila miradi iliyotekelezwa kuzinduliwa bila kujalisha thamani ya pesa inayoendana na miradi halisi.

" Mimi binafsi niliweza kupata bahati ya kukimbiza Mwenge wa Uhuru hapo nyuma kidogo, Tulikuwa hatufanyi ukaguzi makini kama unaofanyika mwaka huu.

Akizungumzia kuhusu kasoro zilizojitokeza katika miradi ya mwaka huu, Mhe.Kanyasu amesema kasoro zote zilizojitokeza mwaka huu hazitajirudia katika Halmashauri hiyo, hivyo ameahidi kuzifanyia kazi.

Katika hatua nyingine, Mhe, Kanyasu amesema  mkoa wa Gieta ni nyumbani kwa Mhe, Rais, Joseph Pombe Magufuli hivyo mwaka ujao atahakikisha hakuna miradi wowote utakaotaliwa kwa vile ni aibu kwao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post