CHENGE AAGIZA SERIKALI KUTOA TAARIFA KUPOTEA KWA MDUDE CHADEMA


Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, ameitaka Serikali kufuatilia na kutoa taarifa za kutekwa kwa kijana na kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mdude Nyagawa ambaye anadaiwa kutekwa.

Mdude anadaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana kwenye ofisi yake Mbozi, mkoani Songwe juzi, Mei 4 wakiwa na silaha za moto.

Chenge ametoa maelekezo hayo bungeni jijini Dodoma leo Jumatatu Mei 6, wakati akijibu hoja ya Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa aliyetoa hoja ya kuahirisha Bunge kwa kutumia kanuni ya 64 kuhusu kujadili jambo la dharura.

Katika hoja yake, Msigwa alisema hivi karibuni kumekuwapo na matukio ya watu kutekwa, kupotea na hata kuuawa, huku akitolea mfano madai ya kutekwa kwa kada wa chama hicho, Mdude.

Akitoa maelezo ya hoja hiyo, Chenge ameitaka Serikali kutolea ufafanuzi jambo hilo.

“Ni kweli suala lolote linalohusu uhai wa binadamu, itakuwa vizuri Serikali itoe maelezo ili wananchi wajue hali ilivyo,” amesema Chenge.

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusufu Masauni amesema Jeshi la Polisi limeanza kufanyia uchunguzi tangu jana, Mei 5, na wameongeza nguvu kutoka makao makuu ya jeshi hilo lakini akapinga madai ya Mdude kutekwa.


"Mbunge Msigwa amesema kuwa Mdude Chadema ametekwa na Polisi wamekataa kufungua jarada kitu ambacho sio sahihi, ukweli wa mtu huyu hakuonekana na ukisema ametekwa inamaana wewe unajua na bila shaka Msigwa ana taarifa hizo na nilielekeze Jeshi la Polisi limtafute Msigwa ili aisaidie Polisi” Amesema Hamad Massauni


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527