ARIF TANZANIA ATAKA WENYE KIPATO KUSAIDIA WASIO NA KIPATO


Na Shushu Joel,Chalinze.

Taasisi ya Miraj Islamic Centre yenye makao yake mkuu jijini Dar es Salaam imetoa wito kwa watu wote walio na nafasi ya kipato kuwasaidia wasio na kipato kama ilivyoagizwa katika vitabu vya Mungu.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa taasisi hiyo Sheikh Arif Yusuf Abdulrehman maarufu Arif Tanzania alipokuwa akizungumza na baadhi ya waislamu wakati wa zoezi la kuwagawia futari wakazi wa Vikindu wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani. 

Arif Tanzania alisema taasisi yake imekuwa miongoni mwa taasisi za kuigwa nchini na nje kwa jinsi inavyojitolea kuwasaidia Watanzania wote pasipo kujali dini zao wala kabila huku lengo likiwa ni kuwaonyesha wale wasio na uwezo kuona ni sawa na wenye uwezo.

"Unaposaidia wenzako Mwenyekiti Mungu anakuongezea kutokana na jinsi wale unaowasaidia wanakuombea uweze kupata ili uendelee kuwasaidia zaidi",alisema Arif Tanzania.

Aliongeza kuwa kwa kipindi hiki cha mwezi huu wa Ramadhan taasisi ya Miraj Islamic imewezesha sehemu mbalimbali kwa ajili wananchi vyakula na tende kwa baadhi ya mikoa kama vile Arusha,Pwani,Mwanza,Kigoma,Zanzibar na mikoa mingine kwa kusudi la kuwasaidia wasio na uwezo wa kipato ila wamefunga katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan. 

Aidha alisema Taasisi yake imekuwa msaada mkubwa kwa serikali kutokana na jinsi inavyojitoa katika masuala ya kusaidia watu mbalimbali ili waweze kujikwamua katika maisha yao,watu hao ni pamoja na kuwasaidia usafiri walemavu,vijana kuwapatia mashine za kukamulia juisi na wengine kuwapatia pikipiki kwa ajili ya kufanya shughuli za boda boda, akinamama kuwawezesha kwa vyerehani ya ushonaji.

Alisema kama kila mwenye nafasi ya kipato akijitolea kwa moyo mmoja basi Watanzania wengi watafikiwa na kuwawezesha ili nao waondokane na umaskini walionao.

Arif Tanzania pia aliipongeza serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi inavyofanya kazi zake na viongozi wa dini zote na kuwakomboa watanzania wa hali za chini kwenye imani zao pasipo kubagua. 

Kwa upande wake Ashura Juma (81) mkazi wa Vikindu katika wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani aliipongeza taasisi ya Miraj Islamic Centre kwa jinsi inavyojitolea katika kutoa misaada mbalimbali kwa wanyonge.

Aliongeza kuwa kwa kipindi hiki cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kupitia taasisi hiyo familia yake imekuwa moja ya wanufaikaji wakubwa kwa kupata misaada mingi ikiwemo chakula kwa ajili ya futari,fedha na mahitaji mengine mengi ya kibinadamu.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa halmashauri ya Chalinze katika wilaya ya Bagamoyo, Mbunge wa jimbo hilo Ridhiwani Kikwete amesema kuwa misaada hiyo inayotolewa na taasisi hiyo imekuwa na tija kubwa kwa waumini wa dini ya kiislamu kutokana na uhitaji wa futari kwenye kipindi hiki.

Mbali na hilo Kikwete alisema pongezi hizo si kwa wananchi bali hata serikali imekuwa ikinufaika na Arif Tanzania kupitia taasisi zake zinazojitolea kwenye maeneo mbalimbali kwa ajili ya wanyonge.

"Kutokana na jinsi taasisi hii inavyojitolea katika ufanikishaji wa wa misaada ni lazima sisi kama wawakilishi tuisemee vizuri ili wengine wajitokeze "alisema .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527