UFAFANUZI KUHUSU HABARI INAYOHUSU UJENZI WA STENDI YA MABASI NJOMBE


Mpendwa Msomaji wetu, Jana Ijumaa April 19,2019 tulichapisha Habari  inayohusu  ujenzi wa Stendi ya Mabasi Njombe iliyokuwa na kichwa cha habari; "Mwanzinga:  Agizo La Rais Magufuli Kukamilishwa Kituo Cha Mabasi Njombe Mjini Ndani Ya Siku 30 Haliwezi Kufanikiwa."

Habari  hiyo ilinukuu mahojiano kati ya mwandishi wetu na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa  Njombe Ndg. Edwin Mwanzinga  kuhusu  maendeleo ya ujenzi wa stendi mpya ya Njombe na namna walivyojipanga kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania  Dr. John pombe Magufuli  ambaye  April 10, 2019 aliagiza  ujenzi wa kituo hicho  ukamilike ndani ya siku 30.

Hata hivyo, katika mahojiano hayo, pamoja na  Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa  Njombe Ndg. Edwin Mwanzinga kuelezea maendeleo ya mradi huo, lakini alinukuliwa vibaya kwamba ujenzi huo unaweza usikamilike kwa  asilimia 100 ndani ya muda walioagizwa na Rais Magufuli.

Tunaomba radhi  kwa makosa hayo ya kiufundi yaliyojitokeza.

Uhalisia wake ni kwamba, Ndg. Edwin Mwanzinga  alifafanua kuwa stendi hiyo itakamilika kwa mujibu wa tarehe ya mkataba ambayo ni 30/04/2019 na shughuli zitakazosalia za ukamilishaji zitafanyika ndani ya siku zilizoongezwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kama alivyoagiza kwenye ziara yake ya kikazi tarehe 10 Aprili akiwa Mkoani Njombe ambapo ni kufikia tarehe 10, Mei 2019.

Ujenzi wa kituo hicho cha mabasi unaotarajia kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 9  ulianza kujengwa  tangu mwaka 2013.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527