Picha : DC KISHAPU AZINDUA MRADI WA SAUTI YA MWANAMKE NA MTOTO WA AGAPE


Mkuu wa wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga bi. Nyabaganga Talaba akipokea nyaraka za mradi wa 'Sauti ya Mwanamke na Mtoto' kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Agape ACP, John Myola (kulia) wakati wa uzinduzi wa mradi huo leo Aprili 9,2019 - Picha na Kadama Malunde - Malunde1 blog
 ***
Mkuu wa wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga Nyabaganga Talaba amezindua rasmi Mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto unaotekelezwa na Shirika la Agape ACP kwa lengo la kumwezesha mwanamke na mtoto kupata haki na usawa kwa wakati katika jamii.


Mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la United Nations Development Programme (UNDP) utatekelezwa kwa kipindi cha miezi sita katika kata tatu za wilaya ya Kishapu ambazo ni Itilima,Bunambiyu na Kishapu.

Akizungumza leo Jumanne Aprili 9,2019 wakati akizindua Mradi huo katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu,Mkuu wa wilaya ya Kishapu,Nyabaganga Talaba alisema mradi huo unalenga kumuinua,kumtetea mwanamke na mtoto.

“Sauti ya mwanamke na mtoto siyo sauti ya kawaida,ni sauti ambayo ikisikika jamii hushtuka, mradi huu uwe chachu ya kuleta mabadiliko kwa wanawake na watoto, wajihisi kuwa wao ni watu wa muhimu sana katika taifa hili,tubadilike pale tulipojisahau na kusahau sauti za makundi haya,sauti, wale waliofanya wanawake na watoto wakose upendo na furaha waache sasa”,alisema Talaba.

“Nawashukuru UNDP kwa kuwezesha mradi huu kufanyika katika wilaya yetu,naomba wasichoke na sisi kama serikali tutahakikisha kuwa tupo bega kwa bega na Agape kuhakikisha malengo ya mradi yaliyokusudiwa yanafikia mwisho”,alisema Talaba.


Alisema hatutaweza kufikia malengo ya serikali ya kufikia uchumi wa kati kama mwanamke bado hajitambui huku akibainisha kuwa mwanamke akijitambua na taifa litajitambua lakini pia maendeleo hayaji kwa kumuacha mwanamke nyuma.

Kwa upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Agape ACP, John Myola alisema mradi huo unalenga kuboresha na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora ya haki na kwa wakati muafaka miongoni mwa wanawake na watoto pamoja na kuimarisha mfumo mzima wa haki za jinai kwa upatikanaji wa haki za jinai kwa watuhumiwa na wahanga/waathirika wa makosa ya jinai.

“Shirika la Agape ACP litashirikiana na wadau mbalimbali ngazi ya mkoa na halmashauri ya wilaya ya Kishapu kupitia idara zake za ustawi wa jamii, maendeleo ya jamii, sheria, viongozi ngazi ya kata na vijiji, polisi kitengo cha dawati la jinsia na watoto, mahakama na ofisi ya mwendesha mashitaka wa serikali, pamoja na Baraza la Watoto la Wilaya ya Kishapu”,alisema Myola.

Aidha alieleza kuwa mradi huo utatelekezwa kwa kipindi cha miezi sita kwa majaribio katika kata ya Kishapu,Itilima na Bunambiyu na kama mafanikio yataonekana maeneo ya utekelezaji wa mradi yanaweza kuongezwa hivyo kuwataka viongozi wa serikali na jamii kwa ujumla kushirikiana na Agape ili kufanikisha mradi huo.

Naye Msimamizi wa mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto, Felix Ngaiza aliyataja matarajio ya mradi kuwa ni kuongezeka uelewa na ufahamu kuhusu sheria na haki miongoni mwa wanajamii ikiwemo ongezeko la taarifa za kesi za ukatili na uvunjifu wa haki za jinai kwa wanawake na watoto.

Alisema mradi huo pia utachangia katika kufikia lengo la Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) la kufikia 50% ifikapo mwaka 2022.

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mkuu wa wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga bi. Nyabaganga Talaba akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa mradi wa 'Sauti ya Mwanamke na Mtoto' unaotekelezwa na shirika la Agape ACP katika kata ya Kishapu,Itilima na Bunambiyu wilayani Kishapu.Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Agape ACP, John Myola. - Picha na Kadama Malunde - Malunde1 blog.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga bi. Nyabaganga Talaba akijiandaa kukata utepe ishara ya uzinduzi wa mradi wa 'Sauti ya Mwanamke na Mtoto' unaotekelezwa na shirika la Agape ACP. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Agape ACP, John Myola. 
Mkuu wa wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga bi. Nyabaganga Talaba akikata utepe wakati wa uzinduzi wa mradi wa 'Sauti ya Mwanamke na Mtoto' .
Mkuu wa wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga bi. Nyabaganga Talaba akipokea nyaraka za mradi wa 'Sauti ya Mwanamke na Mtoto' kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Agape ACP, John Myola.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Agape ACP, John Myola akimonesha Mkuu wa wilaya ya Kishapu,Nyabaganga Talaba Andiko la Mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Agape ACP, John Myola akielezea lengo la mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto na kueleza kuwa walengwa ni wanawake wenye umri wa miaka18-55 na watoto wenye umri wa miaka 7- 17. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Underson Mandia akifuatiwa na Mkuu wa wilaya ya Kishapu,Nyabaganga Talaba.
Msimamizi wa mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto, Felix Ngaiza akitambulisha mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto.
Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Joseph Swalala akiwataka Maafisa watendaji wa kata na vijiji kutoa ushirikiano katika kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake kwani baadhi yao wamekuwa wakituhumiwa kukwamisha kesi kwa kuendekeza vitendo vya rushwa na kukwepesha ukweli.
Wadau wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa uzinduzi wa mradi huo.
Wadau wakiwa ukumbini.
Wadau mbalimbali wakiwa ukumbini wakati wa uzinduzi wa mradi wa Sauti ya Mwanamke na Mtoto.
Wadau wakiwa ukumbini.
Uzinduzi wa mradi unaendelea.
Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Shinyanga, Glory Mbia akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa Sauti ya Mwanamke na mtoto.
Wadau wakiwa ukumbini.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Agape ACP, John Myola akiwaomba wadau katika mradi huo kushirikiana na Agape na serikali kwa kutoa taarifa za matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto badala ya kuwa na tamaa ya pesa.
Afisa Ufuatiliaji,Tathmini na Kujifunza wa Mradi wa Sauti ya Mwanamke na mtoto,Lucy Maganga akisisitiza wadau katika mradi huo kufanya kazi kwa weledi na kutokuwa waoga ili kumkomboa mwanamke na mtoto.
Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Anderson Mandia akisisitiza kuwa madiwani watakuwa mstari wa mbele katika kufanikisha mradi wa Sauti ya Mwanamke na mtoto na kwamba halmashauri ya wilaya ya Kishapu itaendelea kushirikiana na shirika la Agape ili kuhakikisha kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vinakomeshwa wilayani Kishapu.
Picha ya pamoja baada ya uzinduzi wa mradi wa Sauti ya Mwanamke na mtoto.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527