CCM KIBONDO YAAGIZA MRADI WA MAJI ULIOKWAMA TANGU 2014 KAGEZI NA MLANGE UKAMILIKE NDANI YA MWEZI MMOJA

Wananchi wa vijiji vya Kagezi na Mlange Wilayani Kibondo Mkoani Kigoma, wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita mbili kufuata maji katika chanzo cha maji kutokana na mradi wa maji uliogharimu zaidi ya bilioni moja kutokamilika tangu mwaka 2014 hadi sasa.

Wakizungumza jana kijijini hapo wakati wa ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani kwa baadhi ya miradi ya serikali uliofanya na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali ya wilaya hiyo, baadhi ya wananchi hao waliokuwa wakigombania maji katika chanzo cha mto Kagezi, walisema wanapata shida sana ya kuchota maji na hasa ukizingatia Mlima uliopo katika chanzo hicho unawachosha.

Mmoja wa wananchi hao,Agnes Kunjira alisema wanalazimika kuamka asubuhi sana kuwahi kuchota maji ndipo waende mashambani, kutokana na kero hiyo wanashindwa kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa wakati kwa kuwa maji ni uhai na wanahitaji maji.

Aidha aliiomba serikali kufuatilia kwanini mradi huo hautoi maji kwa kuwa kero waliyonayo inawatesa sana na endapo mradi huo ukikamilika na wakaanza kuchota maji vijijini itawasaidia kwa kiasi kikubwa kufanya shughuli zao za maendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Kagezi mwenyekiti wa kijiji hicho,Zabroni Ntimba, alisema tangu mradi huo uanze kujengwa ni muda mrefu na mpaka sasa ulitakiwa uwe umekamilika lakini mwaka 2018 wananchi walipata maji kwa muda wa miezi mitatu tu na baada ya hapo maji hayakutoka tena.

Alisema wananchi wanalalamika sana na hasa kwa kuwa walichangia asilimia 20% ya mradi hali hiyo inasababisha wananchi kushindwa kuchangia hata shughuli zingine za maendeleo, kwa kuwa wamechangia mradi wa maji lakini hawaoni mradi ukifanya kazi.

Akitoa ufafanuzi juu ya mradi huo Mhandisi wa maji wilaya ya Kibondo Michael Nguruwe alisema mkandarasi wa mradi huo aliingia mkataba ,wa shilingi bilioni moja na milioni (244,629,764/=)  mradi ulitakiwa kuwa umekamilika 2014 lakini kutokana na changamoto ya fedha kulipa kwa wakati kwa mkandarasi mradi uliongezewa muda hadi 2018 lakini mpaka sasa haujakabidhiwa kwa wananchi.

Alisema tatizo kubwa lililopelekea mpaka sasa mradi huo kutokamilika kwa wakati, ni changamoto ya mfumo wa umeme, ambalo mkandarasi alishindwa kulikamilisha na kama halmashauri wamezuia kiasi cha shilingi milioni 50 kwa ajili ya umaliziaji wa mradi huo.

Alisema mpaka sasa wanaendelea kutafuta mkandarasi wa mfumo wa umeme katika mradi huo kwa ajili ya kuweka kifaa kitakachosaidia kuongoza mfumo wa umeme katika mradi huo na mradi ukabidhiwe kwa wananchi kwa ajili ya kutumika.

Kutokana na changamoto zilizopo katika mradi huo na kero wanayoipata wananchi, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Kibondo Hamisi Tahilo alisema chama kinaagiza mradi huo kukamilika kwa kipindi cha mwezi mmoja na baada ya mwezi mmoja watafika katika mradi huo kuangalia kama kweli wananchi wameanza kupata maji.

Alisema serikali imetoa zaidi ya bilioni moja kwa ajili ya mradi wa Wananchi lakini hadi sasa mradi huo haujakamilika, serikali iliahidi kuhakikisha wanamtua mama ndoo kichwani ni lazima watendaji kuhakikisha wanasimamia miradi ya serikali inafanyiwa kazi.

"Serikali iliyopo madarakani ni ya CCM na fedha zinatolewa kwa ajili ya kukamilisha miradi wananchi wataiamini serikali baada ya kuona miradi hii inakamilika niombe ndani ya mwezi huo mmoja mradi huu uwe umekamilika", alisema Tahilo.

Hata hivyo aliwaomba wananchi kuwa na subira na kuendelea kujenga imani na CCM kwa kuwa imejipanga kuhakikisha wananchi wote wa vijijini na mijini wanapata huduma sawa sawa na wanaondokana na changamoto zote.

Na Rhoda Ezekiel Kigoma - Malunde1 blog

Baadhi ya wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Kibondo wakiwasaidia wananchi kubeba maji.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kagezi wakichota maji katika chanzo cha mto Kagezi baada ya kero kubwa ya maji kijijini humo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post