MTAMBO WA KUBANGUA KOROSHO WAUA NA KUJERUHI WAWILI AKIWEMO MWANAJESHI LINDI


Mtambo ulioua na kujeruhi

Mtu mmoja amefariki na wengine wawili akiwemo Mwanajeshi kujeruhiwa, kufuatia ajali iliyosababishwa na kulipuka kwa mtambo wa kuchemshia korosho katika eneo la kiwanda cha SIDO mjini Lindi.

Akizungumza kutokea eneo la tukio, Kamanda wa polisi mkoa wa Lindi, Prudensiana Protas, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema chanzo kikubwa ni mtambo wa kubangulia Korosho kulipuka wakati mafunzo ya ubanguaji bora wa korosho yakiendelea.

"Tukio limetokea eneo hili majira ya saa tano asubuhi siku ya Alhamisi, 11 April 2019, ambapo wanafunzi walikuwa na wataalamu wa kufundisha namna bora ya kubangua korosho", amesema Kamanda huyo wa polisi na kuongeza kwamba,

"Katika mafunzo hayo wanafunzi walikuwa 13 na wakati mafunzo yanaendelea kwa vitendo ndipo mtambo wa kuchemshia korosho ulipolipuka na kusababisha majeruhi kwa watu watatu miongoni mwa wale waliokuwa wakipata mafunzo, majeruhi wote walipelekwa Hospitali ya Sokoine lakini kwa bahati mbaya mmoja alifariki". 

Kwa upande wake Mganga Mfawindi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Sokoine, Boniphace Lymo amethibitisha kupokea majeruhi wawili huku akisema mmoja ni mwanajeshi na amelazwa akiendelea na matibabu.

"Majeruhi wa kwanza ni Aisha Mohamed mwenye umri wa miaka 30, mkazi wa Nyangao, Halmashauri ya wilaya ya Lindi, yeye amepata majeraha jicho la kulia na amepata matibabu na kurudi nyumbani", amesema Mganga Mfawidhi.

"Majeruhi wa pili ni Amadeusi Uliolio, Mwanajeshi mwenye umri wa miaka 27, mkazi wa Nachingwea na inasemekana alikuwa pia kwenye mafunzo hayo, yeye amepata majeraha sehemu za miguu yake yote miwili na bado anaendelea na matibabu, ameshonwa sehemu za majeraha ili kuzuia damu isiendelee kuvuja na amelazwa wodi ya upasuaji ya wanaume", ameongeza.

Aidha Mganga Mfawidhi amethibitisha pia kutokea kwa kifo cha Saada Juma ambaye amesema kimesababishwa na marehemu kuvuja kwa damu nyingi na kukosa hewa.

"Tumepokea pia mwili wa Saada Issa Juma (28), mkazi wa Msinjahili Manispaa ya mji wa Lindi, yeye amepata majeraha makubwa eneo la shingo na koo baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali,ikasababisha kuvuja damu nyingi na kukosa hewa hivyo kupelekea kifo chake", amesema Mganga Mfawidhi.

Chanzo- EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post