WANANCHI KAGEZI WAISHUKURU SERIKALI KWA KUWAPATIA KITUO CHA AFYA

Wananchi wa kijiji cha Kagezi wilayani Kibondo Mkoani Kigoma Wameishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kupanua majengo katika Zahanati yao na kuifanya zahanati hiyo kuwa kituo cha Afya kinachotoa huduma zote.

Wananchi hao walisema wamekuwa wakiteseka kutembea mwendo wa masaa manne kufuata huduma wilayani kwa kuwa huduma zilizokuwa zikitolewa katika zahanati ni za awali tu lakini endapo kituo hicho kitakamilika wana hakika ya kupata huduma bora na kupunguza changamoto zilizo kuwepo.

Silvanus Ntabandi ambaye ni Mkazi wa Kagezi alisema mwanzoni wanawake wote walikuwa wanakwenda kujifungulia katika hospitali ya Wilaya, wapo baadhi walikuwa wanapoteza maisha kutokana na kukosa huduma mapema lakini kwa sasa serikali imeamua kujenga kituo cha afya ambacho kitatoa huduma zote.

Aidha aliiomba Serikali kuongeza watumishi na kuhakikisha kituo hicho cha Afya kinafanya kazi siku zote, tofauti na sasa ambapo kituo hicho kinafanya kazi Jumatatu hadi Ijumaa tu na wao wanahitaji huduma hiyo siku zote.

Justina Gerald alisema kwa sasa hali ni safi katika kijiji hicho na huduma zimesogezwa karibu serikali inawajali na kuhakikisha watu wote wanapata huduma karibu na maeneo yao na kuhakikisha hakuna mtu anapoteza maisha kwa kukosa huduma.

Alisema ukifika katika kituo hicho cha afya sasa hivi wanapatiwa dawa zote kwa wakati na watu wanatibiwa tofauti na mwanzo ulikuwa ukiwa na mgonjwa ambaye ana shida sana wanalazimika kumkimbiza hospitali ya wilaya ili aweze kupata huduma.

Hata hivyo aliiomba Serilika kuwasaidia kupata gari lingine la kubebea wagonjwa kwa kuwa gari lililopo linatumiwa na vijiji vitatu na watu ni wengi na wanahitaji gari kwa kipindi hiki ambacho huduma hazijaanza kutolewa iliwaweze kusafirisha wagonjwa wanaoshindwa kupata huduma katika kituo hicho.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa wilaya ya Kibondo Daudi Mapunda ujenzi wa kituo cha afya Kagezi ulianza Februari 2018 na mpaka Juni wanatarajia majengo yawe yamekamilika na kuanza kutoa huduma.

Alisema ujenzi huo umefadhiliwa na serikali ya awamu ya tano, kupitia mfuko wa kuboresha huduma za afya na awamu hii wamepokea kiasi cha shilingi milioni 620 zitakazotumika kujenga jengo la huduma ya baba mama na mtoto, jengo la upasuaji, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la kufulia, jengo la wodi ya watoto , wazazi na jengo la nyumba ya mganga.

Mpaka sasa ujenzi wa kituo hicho cha afya umekamilika kwa asilimia 90% shughuli zilizobaki ni ndogo na katika fedha hizo wanatarajia kuokoa kiasi cha fedha kitakacho baki na kitafanya shughuli nyingine katika kituo hicho.

Mbali na fedha hizo serikali kupitia wakala wa madawa na vifaa tiba wametoa kiasi cha shilingi milion mia nne kwa ajili ya upatikanaji wa vifaa tiba vyote na baada ya majengo hayo kukamili wananchi wataanza kupata huduma zote.

Alisema kituo hicho kikikamilika kitaanza kutoa huduma za Upasuaji na huduma zote za muhimu kwa kuwa vifaa vyote vinaletwa pamoja na wataalamu wa vifaa hivyo.

Hata hivyo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibondo, Hamis Tahilo aliwapongeza wasimamizi wa miradi hiyo na kuwaomba wananchi kutumia vizuri majengo hayo kwa kuwa serikali inajitahidi kuboresha hudima za afya na wananchi wanatakiwa kulinda miundombinu.

Alisema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi iliahidi kuboresha huduma za afya na sasa wamejitahidi kufanya hivyo na kuwaomba wananchi kuendelea kuwa na imani na chama hicho kwa kuwa ni chama kinachowajali wanyonge.
Na Rhoda Ezekiel - Kigoma 
Wajumbe wa kamati ya siasa ya Wilaya ya Kibondo wakiongozwa na Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Kibondo Daudi Mapunda katika ukaguzi wa Kituo cha Afya Kagezi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527