BABA WA KAMBO AMUUA MTOTO KISA MAMA KAKATAA JINA LAKE LISIWEKWE KWENYE CHETI CHA KUZALIWA MTOTO


Polisi mjini Murang'a wanamshikilia mwanaume  Paul Njuguna Njoroge (25) anayedaiwa kumuua mwanawe wa kiume Collins Waweru (5) kwa kumshambulia kwa panga kwa sababu ya cheti cha kuzaliwa cha mtoto.


Inaaminiwa kuwa, mwanaume huyo alimuua mtoto huyo baada ya mama kukataa kujumuisha jina lake katika cheti cha kuzaliwa cha mtoto.

Evans Macharia ni baba halali na jina lake lipo katika cheti hicho lakini Paul Njuguna Njoroge ni baba wa kambo tu

Mwanaume huyo alimuua Collins Waweru akiwa usingizini katika nyumba ya bibi yake katika kijiji cha Kiharu, usiku wa Jumamosi, Aprili 6,2019.

 Makachero walimtia mbaroni Paul Njuguna Njoroge mnamo Jumatano, Aprili 10,2019 katika kituo cha biashara cha Mukarara nchini Kenya. 

Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi Murang'a Josephat Kinyua alisema mshukiwa alizozana kwanza na shangazi wa marehemu ambaye alikuwa akimlea. 

“Alikatwa mkono wake wa kushoto lakini alifanikiwa kutoroka na kupiga mayowe kuwaita majirani," Kinyua alisema. 

Helen Njambi, mama wa marehemu akizungumza na wanahabari wakati akiomboleza kifo cha mwanawe wa miaka mitano.

 Kulingana na polisi, mshukiwa alivizia usiku na kuwashinda nguvu shangazi na bibi wa marehemu ambaye hana uwezo mkubwa wa kuona kabla ya kumuua Collins aliyekuwa amelala. 

Polisi wanasema majirani walifika na kukuta marehemu kitandani huku mpwa wa marehemu waliyekuwa wamelala naye akiwa katika mushtuko mkubwa.

 “Mshukiwa amekiri kutekeleza mauaji hayo na anadai mama wa marehemu alikataa kulijumuisha jina lake katika cheti cha kuzaliwa cha mtoto huyo hata ingawa yeye si baba halali ya marehemu. 

 “Anasema alimlea mtoto huyo na hata ingawa walikuwa hawaishi pamoja ilikuwa ni vyema jina lake kuwa katika cheti hicho ingawa mama alikataa,” mmoja wa maafisa wa polisi ambaye hakutaka jina lake kutajwa alisema.

 Mama ya marehemu hakuwapo wakati wa tukio hilo na alifahamishwa kuhusu kifo cha mwanawe mara baada ya kuwasili nyumbani na kupata hali ya maombolezo ilikuwa imetanda. 

Kufuatia visa vingi vya mauaji na migogoro ya kinyumbani Kaunti ya Murang’a, kamanda wa polisi aliwataka wakaaji kutafuta njia za kiheshima za kusuluhisha migogoro yao bila ya kuua ama kuitawanya familia.

 Mshukiwa alifikishwa kortini Murang’a, Alhamisi, Aprili 11,2019 na kushtakiwa kwa mauaji ila bado anazuiliwa huku uchunguzi ukiendelea. 

Ripoti ya Mark Wachira - Tuko Murang'a 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post