DC WA RUANGWA AWATAKA TAMWA KURUDISHA WATOTO SHULE...APIGA MARUFUKU UNYAGO

Na Bakari Chijumba,Lindi.

katika kuendeleza kusaidia watoto wa kike, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hashim Mgandiliwa  amewaomba Chama cha Wanahabari wanawake Tanzania (TAMWA) kuchukua jukumu la kuwasaidia kuwaendeleza kimasomo watoto walioacha shule na wana nia ya kuendelea na masomo.

Amesema hayo 30 Machi 2019, wakati wa muendelezo wa  kikao cha kujadili jinsi ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kilichofanyika ukumbi wa Rutesco mjini Ruangwa.

"TAMWA bebeni hawa watoto wenye nia  ya kurudi shuleni hawajachelewa wanaweza kusaidiwa na wakafikia malengo yako kama watoto wengine waliopata bahati ya kusoma kwa wakati" amesema Mgandilwa.

Pia amewataka TAMWA kuhakikisha katika kila mikutano yao wanayofanya wanahamasisha wazazi kufanya shughuli za unyago wakati wa likizo ili kutomnyima haki ya mtoto kupata elimu.

"Serikali haipingi unyago mimi pia sipingi unyago hizo ni mila na desturi zipo katika kila kabila nchini, ila mfanye jambo hilo kwa kufuata maelekezo yanayotolewa, narudia serikali haina tatizo na mila na desturi " DC Mgandilwa na kuongeza kuwa;

"Hakuna ujanja zaidi ya elimu Elimu ndiyo kila kitu hata mie kuwa hapa ni kwasababu ya elimu sasa mkitoka hapa nyie wanafunzi mliopata mafunzo haya mkawe mabalozi kwa wenzenu muwaeleze umuhimu na faida ya elimu"

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TAMWA Bi Rose Reuben, amewataka watoto wakike kuamka na kutambua thamani yao na kuacha tabia za kuiga mambo yasiyo na maana katika maisha yao.

"Mkianza kujitambua nyie hata watu wengine wataanza kuwatambua jisimamieni katika vitu vyenye manufaa umeshindwa kumaliza masomo kwa ajili ya ujauzito basi msimamie mtoto uliyenaye aje kuwa kiongozi mkubwa baadae" Amesema Bi Rose

Aidha kwa niaba ya wenzake, Mwanafunzi Amina Omari Makota, ameuomba uongozi kuwachukulia hatua za kisheria wazazi ambao hawawapi ushirikiano watoto wanaoitaji kusoma  na wanapopeleka malalamiko sehemu husika basi mzazi huyo achukuliwe hatua kwa haraka.

Amina amesema siyo watoto wote wanaoacha masomo ni kwasababu hawataki kusoma, wapo wanaoacha kusoma kwasababu wazazi wao hawawatimizi mahitaji muhimu yanayoitajika shuleni .


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post