BENKI YA DUNIA KUIJAZA TANZANIA MKOPO NA MSAADA WA TRILIONI 4


Benny Mwaipaja, WFM, Washington D.C
BENKI ya Dunia imeahidi kuipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu na msaada wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.7 sawa na takriban shilingi trilioni 4 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020.

Ahadi hiyo imetolewa mjini Washington D.C nchini Marekani na Makamu wa Rais wa Benki hiyo anayeshughulikia Kanda ya Afrika Bw. Hafez Ghanem, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango.

Bw. Ghanem amemhakikishia Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwamba uhusiano kati ya Serikali na Benki yake bado uko imara na kwamba benki hiyo iko tayari kushirikiana na Tanzania ili iweze kufikia maendeleo yanayo tarajiwa.

Miongoni mwa miradi itakayonufaika na mkopo na msaada huo ni mpango wa elimu ambapo benki hiyo imeongeza ufadhili kutoka dola milioni 300 hadi dola milioni 400 na mradi wa kusaidia kaya masikini kupitia TASAF ambapo benki hiyo imeamua kuongeza kiwango cha fedha kutoka dola milioni 300 hadi kufikia dola milioni 450.

Kiasi kingine cha fedha kitatumika kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta za miundombinu ya barabara, maji, Tehama, Afya, kilimo, hifadhi ya jamiim Nishati, utawala bora, lishe, sekta ya fedha, biashara, mazingira na maliasili pamoja na maji nk.

Akizungumza kwenye kikao hicho Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameishukuru Benki hiyo namna inavyoisaidia nchi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii ambapo mpaka sasa Benki hiyo imefadhili miradi 21 ya maendeleo kwa gharama ya dola za Marekani bilioni 4.8, sawa na takriban shilingi trilioni 11.

Ameahidi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa masuala mbalimbali na kuiomba benki hiyo iendelee kuisaidia nchi ili iweze kufikia maendeleo yaliyokusudiwa ikiwemo kuondoa umasikini wa  wananchi.

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, ukimshirikisha pia Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga, upo mjini Washington D.C nchini Marekani kuhudhuria mikutano ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, taasisi ambazo Serikali ina hisa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post