ALMASI KUBWA KULIKO ZOTE YAPATIKANA SHINYANGA....HAIJAWAHI KUTOKEA

Almasi yenye ukubwa wa karati 521 imepatikana katika mgodi wa Mwadui Mkoani Shinyanga tangu mgodi huo uanze uzalishaji miaka 87 iliyopita.

Akitoa taarifa hiyo Ofisini kwake mbele ya waandishi wa Habari leo tarehe 30 Aprili, 2019, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amesema almasi hiyo itauzwa ndani ya nchi ili kodi itakayopatikana ibaki katika mkoa wa Shinyanga na nchini.

"Ni almasi kubwa ambayo haijawahi kupatikana kwenye Mkoa wetu hususani katika Mgodi wa Mwadui ambao ni wa zamani sana, ni fahari kubwa kwa Mkoa wetu" amesema Mhe. Telack.

Mhe. Telack ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara wote wa Almasi kuja kununua katika mkoa wa Shinyanga ambapo tayari soko la madini katika Wilaya ya Kahama linaendelea vizuri wakati soko jingine la madini litafunguliwa katika Wilaya ya Shinyanga hapo tarehe 3 Mei, 2019.

Aidha, ametoa wito kwa wafanyabiashara wote ndani ya Mkoa kuendelea kutumia masoko yaliyoandaliwa kwa ajili ya uuzaji wa madini, waache kununua katika maeneo yasiyo rasmi.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akionesha almasi hiyo. Almasi hii ndiyo yenye uzito mkubwa kupatikana katika mgodi wa Mwadui uliopo Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga tangu mgodi hio uanzishwe miaka zaidi ya 80 iliyopita. Almasi hii yenye ukubwa wa karato 521 itauzwa ndani ya masoko ya madini ndani ya Mkoa wa Shinyanga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527