SIMBA YATEMBEZA KICHAPO KWA WAKONGO AS VITA...YATINGA ROBO FAINALI LIGI YA MABINGWA


Simba SC imefanikiwa kwenda Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) usiku huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Shujaa wa Simba SC leo ni kiungo Mzambia, Clatous Chama aliyefunga bao la ushindi dakika ya 90 akimalizia pasi ya Nahodha, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, John Raphael Bocco aliyesogeza krosi ya kiungo Mnyarwanda, Haruna Hakizimana Niyonzima.

Na hiyo ilifuatia AS Vita kutangulia kwa bao la Francis Kazadi Kasengu dakika ya 12 akimalizia mpira uliozuiwa na beki Muivory Coast wa Simba SC, Serge Wawa Pascal baada ya shuti la Fabrice Ngoma.

Ikawachukua Simba SC dakika 24 kusawazisha bao hilo kupitia kwa beki wake wa kushoto na Nahodha Msaidizi wa klabu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ aliyewazidi mbio mabeki wa AS Vita dakika ya 36 baada ya kutanguliziwa pasi na kiungo Muzamil Yassin.

AS Vita walianza kucheza kwa tahadhari baada ya bao hilo, huku Simba SC ikiongeza kasi ya mashambulizi kusaka bao la ushindi hadi walipofanikiwa.

Na kwa ujumla kipindi cha pili, AS Vita walizidiwa na Simba SC hususan baada ya mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mbelgiji, Patrick Aussems akiwatoa Emmanuel Okwi, Muzamil Yassin na James Kotei na kuwaingiza Haruna Niyonzima, Rashid Juma na Hassan Dilunga.

Mchezo mwingine wa Kundi D, Al Ahly imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JS Saoura mabao ya Fateh Talah aliyejifunga dakika ya 30, Marwan Mohsen dakika ya 45 na ushei na Hussein El Shahat dakika ya 81.

Ahly inamaliza kileleni mwa Kundi D kwa pointi zake 10, ikifuatiwa na Simba SC yenye pointi tisa, wakati JS Saoura ni ya tatu kwa pointi zake nane na AS Vita imeshika mkia kwa pointi zake saba.

Kikosi cha Simba SC kilikuwa: Aishi Manula, Zana Coulibally, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Serge Wawa, James Kotei/Rashid Juma dk84, Clatous Chama, Muzamil Yassin/Hassan Dilunga dk77, John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi/Haruna Niyonzima dk57. 

AS Vita: Nelson Lukong, Shabani Djuma, Yannick Bangala, Bompunga Botuli Padou, Ernest Luzolo Sita, Nelson Munganga, Tuisila Kisinda/Ducapel Moloko dk61, Glody Ngonda, Fabrice Luamba Ngoma, Francis Kazadi/Jeremie Mumbere dk75 na Jean-Marc Makusu/Cesar Lobi Manzoki dk64.

Via>>Binzubeiry

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post